Wabahrain waandamana kumuunga mkono Sheikh Isa Qassim
Maelfu ya wananchi wa Bahrain wameandamana kote katika ufalme huo kwa siku ya pili mfululizo wakipinga kukandamizwa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Isa Qassim.
Katika maandamano ya Alhamisi usiku, waandamanaji walikusanyika katika Medani ya al-Fada kaskazini magharibi mwa kijiji cha Diraz iliko nyumba ya Sheikh Qassim.
Maandamano hayo yalikuja masaa machache baada ya vyombo vya mahakama nchini humo kuakhirisha tena kesi ya mwanazuoni huyo hadi baadaye mwezi huu wa Januari. Kwa karibu siku 200 sasa, wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga kuvuliwa uraia Sheikh Isa Qassim kwa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti anachochea malumbano ya kimadhehebu na ghasia. Sheikh Qassim, aliyevuliwa uraia mwezi Juni mwaka jana, ni mashuhuri kwa misimamo yake ya kutetea Umoja wa Kiislamu na maandamano ya amani Bahrain.
Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.