Jeshi la Tunisia laungana na jeshi la Syria kupambana na magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25083-jeshi_la_tunisia_laungana_na_jeshi_la_syria_kupambana_na_magaidi
Duru za kuaminika za Tunisia zimesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limetumwa nchini Syria kupambana bega kwa bega na serikali ya Syria dhidi ya magenge ya kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 13, 2017 15:10 UTC
  • Wananchi wa Syria wakisherehekea kukombolewa mji muhimu wa Halab (Aleppo) kutoka mikononi mwa magenge ya kigaidi.
    Wananchi wa Syria wakisherehekea kukombolewa mji muhimu wa Halab (Aleppo) kutoka mikononi mwa magenge ya kigaidi.

Duru za kuaminika za Tunisia zimesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limetumwa nchini Syria kupambana bega kwa bega na serikali ya Syria dhidi ya magenge ya kigaidi katika ardhi ya nchi hiyo.

Shirika rasmi la habari la Tunisia limetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa Tunisia chini ya kikosi kinachojulikana kwa jina la Gadi ya Taifa ya Waarabu, hivi sasa wanapigana bega kwa bega na jeshi la Syria dhidi ya magaidi wanaofanya jinai za kila namna nchini Syria.

Kikosi hicho cha cha Gadi ya Taifa ya Waarabu kiko chini ya jeshi la Syria na kinaundwa na wanajeshi kutoka Tunisia, Algeria, Lebanon, Misri, Palestina na Jordan.

Wakati huo huo Basil al Kharrat, afisa wa masuala ya kisiasa wa Gadi ya Taifa ya Waarabu huko Halab (Aleppo) kaskazini mwa Syria amesema, wananchi wa Tunisia wako pamoja na wananchi wa Syria katika vita dhidi ya magaidi.

Wanajeshi wa Tunisia wakiwa kwenye operesheni maalumu

 

Ikumbukwe kuwa idadi kubwa ya raia wa Tunisia walimiminika nchini Syria kujiunga na magenge ya kigaidi kama vile Daesh (ISIS) na Jabhat an Nusra kufanya mauaji na jinai dhidi ya raia na maafisa wa serikali ya Syria.

Kwa upande wake, gazeti la al Akhbar la Lebanon hivi karibuni liliripoti kuwa, kikosi kimoja cha wahandisi wa jeshi la Misri kimetumwa katika maeneo yaliyokombolewa huko Halab Syria kwa ajili ya kuyasafisha maeneo hayo na mabomu yaliyotegwa ardhini na magaidi.

Zaidi ya miaka mitano sasa Syria inapambana na magenge ya kigaidi yanayopata uungaji mkono kutoka madola ya kibeberu yakisaidiwa na baadhi ya nchi jirani na za Kiarabu kama vile Saudi Arabia na Uturuki.