Saudia yakubali masharti ya Iran kuhusu ibada ya Hijja
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25880-saudia_yakubali_masharti_ya_iran_kuhusu_ibada_ya_hijja
Saudi Arabia imekubali mapendekezo yalitolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kulindwa mahujaji wa taifa hili katika ibada ya Hijja.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 03, 2017 08:12 UTC
  • Saudia yakubali masharti ya Iran kuhusu ibada ya Hijja

Saudi Arabia imekubali mapendekezo yalitolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kulindwa mahujaji wa taifa hili katika ibada ya Hijja.

Hamid Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Kushughulikia Masuala ya Hijja ya Iran amesema duru kadhaa za mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Tehran na Riyadh kuhusu ibada hiyo tukufu zimepiga hatua chanya.

Mohammadi ambaye aliongoza ujumbe wa Iran huko Riyadh wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na Waziri wa Hijja na Umra wa Saudia amesema kuwa, vikao hivyo vilijikita zaidi katika masuala ya kuheshimiwa Mahujaji wa Kiirani na kudhaminiwa usalama wao katika ibada hiyo.

Amesema Riyadh imekubali ramani ya njia iliyopendekezwa na Tehran kuhusu utata uliopo, ambapo mbali na Mahujaji wa Kiirani kustafidi na huduma za afya wakiwa katika ibada hiyo, Saudia imesema kuwa maafisa wawili wa polisi waliowadhalilisha Mahujaji wa Kiirani mjini Jeddah mwaka 2015, tayari wamehukumiwa.

Miili ya wahanga wa mkasa wa Mina mwaka 2015

Mwaka jana 2016, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikushiriki ibada tukufu ya Hijja kutokana na vizingiti ilivyowekewa na Saudi Arabia na utawala wa Riyadh kushindwa kushughulikia matakwa yake.

Itakumbukwa kuwa, Mahujaji zaidi ya 4,700, ambapo 460 miongoni mwao walikuwa raia wa Iran, waliaga dunia kutokana na usimamizi mbaya wa ibada hiyo tukufu katika eneo la Mina mwaka 2015. Hata hivyo Riyadh ilidai kuwa ni watu 770 tu ndio walipoteza maisha katika mkanyagano huo.