Jibu baridi la Utawala wa Kizayuni kuhusu kuenea vikwazo dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26072-jibu_baridi_la_utawala_wa_kizayuni_kuhusu_kuenea_vikwazo_dhidi_yake
Kufuatia kuimarika harakati ya kimataifa ya kuususia na kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel, bunge la utawala huo limepitisha sheria kuwazuia waungaji mkono wa vikwazo hivyo kuingia katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 07, 2017 23:49 UTC
  • Jibu baridi la Utawala wa Kizayuni kuhusu kuenea vikwazo dhidi yake

Kufuatia kuimarika harakati ya kimataifa ya kuususia na kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel, bunge la utawala huo limepitisha sheria kuwazuia waungaji mkono wa vikwazo hivyo kuingia katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Wakati wa kupitisha sheria hiyo, bunge la utawala wa Israel limesema vikwazo na ususiwaji ni wigo mpya wa vita dhidi ya Israel na limetaka hatua zichukuliwe kukabiliana na hali hiyo. Kwa mujibu wa sheria hiyo, watu au wawakilishi wa makundi yanayounga mkono vikwazo dhidi ya Israel wanapaswa kupigwa marufuku kuingia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni na wakuu wa utawala huo vimekuwa shadidi na Wazayuni wenyewe wamekiri kuwa vikwazo hivyo vimewadhuru na wanatafuta kila njia kujikwamua kutoka katika mkwamo huo.

Harakati ya Vikwazo,  Kususia na Kuzuia Uwekezaji Israel (BDS) ni harakati ya kimataifa yenye lengo la kuushinikiza utawala haramu wa Israel kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa lengo la kuushurutisha usitishe ukaliwaji wake kimabavu wa ardhi za Palestina na pia kuutaka usitishe ubaguzi na utambue rasmi hali ya mamilioni ya wakimbizi Wapalestina kurejea katika ardhi zao. Hivi sasa nchi kadhaa zimeunda kampeni ya kususia bidhaa za Israeli  na jambo hilo limewatia kiwewe na wasi wasi wakuu wa utawala wa Kizayuni kwani kampeni hiyo inazidi kupanuka kila siku.

Wananchi wa Ufaransa katika maandamano ya kutaka Israel isusiwe

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni umezidi kutengwa kimataifa na hata sasa nchi za Ulaya zimejiunga na kampeni hiyo ya kuususia na kuutenga utawala huo dhalimu.

Sababu ya kutengwa utawala huo wa Kizayuni ni kutokana na kushadidi jinai zake  na uporaji ardhi za Wapalestina.

Waliwmengu wametoa jibu lao kwa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina kwa kushiriki katika maandamano dhidi ya utawala wa Kizayuni katika kila kona ya dunia hata katika nchi za Ulaya.

Katika miaka ya hivi karibuni, kila tarehe 6-18 mwezi Machi huadhimishwa Wiki ya Kupinga Utawala wa Ubaguzi wa Israel ambapo washiriki hujumuika pamoja na kulaani sera za kujitanua za utawala wa Kizayuni ambao msingi wake ni ubaguzi wa rangi, kaumu na dini. Utawala haramu wa Israel unafananishwa na utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) ulioangushwa Afrika Kusini.

Kuenea na kupanuka wigo wa harakati za kupinga Israel kumekuwa na taathira kubwa kiasi kwamba mwaka 2016 kulishuhudiwa maandamano katika miji 225 kote duniani ambapo waandamanaji walitangaza bayana upinzani wao kwa utawala wa kibaguzi wa Israel.

Harakati hizi za walimwengu sambamba na kukusanywa misaada ya umma kwa ajili ya kuwasaidia Wapalestina wanaokandamizwa na Israel hasa katika Ukanda wa Ghaza zinaitaka dunia iuwekee vikwazo utawala wa Kizayuni.

Hivi sasa serikali za Ulaya ziko chini ya mashinikizo ya fikra za umma kuchukua hatua za kivitendo kuuwekea vikwazo vya kiuchumi utawala huo wa Kizayuni.

Mwaka 2013, Umoja wa Ulaya ulipitisha sera ya kuzuia umoja huo kusaidia kifedha miradi ya Israeli iliyo katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ambavyo vimejengwa katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Quds Mashariki na Miinuko ya Golan. Aidha Umoja wa Ulaya ulipiga marufuku ununuzi wa bidhaa zilizozalishwa katika vitongoji hivyo. Hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya imekuwa na taathira hasi za kiuchumi kwa  utawala huo.

Uharibifu uliosababishwa na Israel katika Ukanda wa Ghaza

Wataalamu wa masuala ya Israel wanaamini kuwa  utawala huo unapata hasara ya zaidi ya dola bilioni nane kwa mwaka kutokana na vikwazo na ususiwaji wa kimataifa. Taathira ya vikwazo hivyo inatazamiwa kuwa mbaya kutokana na azimio ambalo lilipitishwa mwezi Disemba dhidi ya Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kulaani ujenzi wa viteongji vya walowezi wa Kizayuni.

Aidha maazimio mengine mengi ya kimataifa dhidi ya Israel na kwa ajili ya kuunga mkono Palestina bila shaka ni chanzo cha kupata hasara kubwa utawala wa Kizayuni. Hakuna shaka kuwa utawala haramu wa Israel utakabiliwa na matatizo  kutokana na kuendelea vikwazo na mashinikizo ya kimataifa dhidi yake. Kuendelea mkondo huu kutapelekea utawala wa Kizayuni kukumbwa na matatizo na changamoto chungu nzima na hivyo kuharakisha mkondo wa kusambaratika kwake. Ni kutokana na hali hii ndipo utawala wa Kizayuni ukachanganyikiwa na kushindwa la kufanya na hivyo kupitisha sheria isiyo na maana ya kuwazuia wanaoususia utawala huo kuingia katika ardhi zilizoghusubiwa. Sheria hiyo imepitishwa kwa ajili tu ya kujaribu kuwatuliza Wazayuni walioingiwa na kiwewe na wala haitakuwa na taathira yoyote ya kivitendo.