Hamas yalaani muswada wa sheria ya Israel wa kuzima adhana Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26222-hamas_yalaani_muswada_wa_sheria_ya_israel_wa_kuzima_adhana_quds
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekosoa vikali muswada wa sheria uliopasishwa hivi karibuni na Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, unaopania kupiga marufuku kusomwa adhana katika misikiti ya Quds tukufu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2017 02:52 UTC
  • Hamas yalaani muswada wa sheria ya Israel wa kuzima adhana Quds

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekosoa vikali muswada wa sheria uliopasishwa hivi karibuni na Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, unaopania kupiga marufuku kusomwa adhana katika misikiti ya Quds tukufu.

 Akihutubu katika Ukanda wa Gaza jana Ijumaa, Ismail Haniya, afisa mwandamizi wa Hamas alisema uamuzi huo wa kichokozi wa Israel kamwe hautafua dafu.  

Haniya ambaye ni Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas ameongeza kuwa: "Liwe liwalo, taifa letu na watu wetu wataendelea kusoma adhana kote duniani." 

Ismail Haniya, afisa mwandamizi wa Hamas

Kauli ya Haniya imetilia pondo matamshi yaliyotolewa siku chache zilizopita na Sheikh Muhammad Ahmad Hussein, Mufti Mkuu wa Baitul Muqaddas ambaye pia ni Imam wa Msikiti wa al-Aqsa ambaye alisema kuwa, katu Wapalestina hawatatambua wala kuheshimu sheria yoyote ya kuhujumu uhuru wao wa kuabudu na kutekeleza ibada zao, itakayopasishwa na Bunge la Israel au chombo chochote cha utawala huo haramu.

Jumatano iliyopita, Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel (Knesset) lilipasisha hatua ya kwanza ya muswada wa sheria inayopiga marufuku adhana katika misikiti ya mji mtakatifu wa Quds kwa kura 55 za ndio na 48 za hapana. Kwa mujibu wa vipengee vya rasimu hiyo, adhana kwa vipaza sauti ni marufuku Quds Tukufu kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi.

Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel, Benjami Netanyahu amesema anaunga mkono kikamilifu muswada huo wa sheria ya kupiga marufuku adhana, akidai kuwa sauti hiyo ya kuwaita Waislamu wakatekeleze ibada yao ya swala inaudhi na ni kero kwenye masikio ya Wazayuni.