Bahrain yaakhirisha tena hukumu dhidi ya Sheikh Isa Qassim
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26376-bahrain_yaakhirisha_tena_hukumu_dhidi_ya_sheikh_isa_qassim
Kwa mara nyingine tena utawala wa Aal-Khalifa umeakhirisha kutolewa hukumu dhidi ya Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain hadi Mei 7 mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 14, 2017 11:24 UTC
  • Bahrain yaakhirisha tena hukumu dhidi ya Sheikh Isa Qassim

Kwa mara nyingine tena utawala wa Aal-Khalifa umeakhirisha kutolewa hukumu dhidi ya Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain hadi Mei 7 mwaka huu.

Hukumu dhidi ya kiongozi huyo wa Kiislamu ilipangwa kutolewa leo Jumanne. Hukumu hiyo imeakhirishwa katika hali ambayo, duru za habari zimedokeza kuwa, utawala wa Manama unapanga kumpeleka uhamishoni nchini Uturuki Sheikh Isa Qassim, kwa lengo la kupunguza taharuki na ghadhabu za wananchi wanaoishinikiza serikali kumuachia huru mara moja.

Tangu usiku wa jana Jumatatu, eneo la Diraz lililoko magharibi mwa mji mkuu wa Bahrain anakotokea msomi huyo wa kidini, limekuwa uwanja wa maandamano na mikusanyiko ya Wabahrain kulalamikia ukandamizaji na uonevu wa utawala wa nchi hiyo dhidi ya mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kishia.

Maandamano ya amani ya kumuunga mkono Sheikh Qassim mjini Diraz

Itakumbukwa kuwa, Septemba 15 vyombo vya mahakama vya utawala dhalimu wa Aal-Khalifa nchini Bahrain viliakhirisha tena kutolewa hukumu dhidi ya Sheikh Qassim, mwanazuoni mashuhuri na mkuu wa kimaanawi wa mapinduzi ya watu wa nchi hiyo, hadi Septemba 26 mwaka huo, kabla ya kuiakhirisha tena. 

Utawala wa kiukoo wa Aal-Khalifa unamtuhumu Sheikh Qassim kwamba amekuwa akieneza chuki za kimadhehebu miongoni mwa watu wa  Bahrain mbali na kuchochea machafuko na kuhatarisha usalama wa taifa.

Kutokana na tuhuma hizo bandia, utawala huo sio tu unaendelea kumzuilia kinyume cha sheria Sheikh Qassim, bali ulimvua uraia wa Bahrain mwanaharakati huyo tarehe 20 mwezi Juni mwaka uliopita 2016, jambo ambalo liliamsha hasira kubwa ya wanachi wa nchi hiyo na wa mataifa mengine huru duniani.