Amnesty yaitaka US ikome kuziuzia silaha Saudia na Bahrain
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Marekani iache kuziuzia silaha serikali za Saudi Arabia na Bahrain kutokana na nchi hizo kutumia silaha hizo kuvunja haki za raia.
Shirika la Msamaha Duniani limemuandikia barua Rais Donald Trump wa Marekani likimtaka asisaini makubaliano ya mauzo mapya ya silaha zake kwa tawala za Aal-Saud na Aal-Khalifa na kuonya kuwa, kitendo hicho kitaitumbukiza Washington katika jinai za kivita.
Amnesty International imesema silaha hizo zikiwemo za mabomu ya vishada ambazo zimepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria za kimataifa, zinatumiwa na Riyadh dhidi ya raia wasio na hatia nchini Yemen.
Wiki iliyopita, tovuti ya Business Insider ya nchini Marekani iliripoti kuwa washington ni muuzaji wa theluthi nzima ya silaha zote zinazonunuliwa katika maeneo mbalimbali duniani.
Kabla ya hapo Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm ilitangaza kuwa, Saudi Arabia ni mnunuzi mkuu wa silaha za Marekani.
Utawala wa kiimla wa Manama kwa msaada wa wanajeshi wa Saudia, nao unatumia mkono wa chuma kukabiliana kila uchao na maandamano ya amani ya wananchi wanaopigania haki zao za kimsingi kabisa huko Bahrain.