Kufichuka ushirikiano mkubwa baina ya Israel na magaidi wakufurishaji
Ripoti zimeenea kuhusu ushirikiano mkubwa uliopo baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na magaidi wenye misimamo mikali ya ukufurishaji.
Kwa mujibu wa televisheni ya Russia ya Roosiya Al Youm inayorusha matangazo kwa lugha ya Kiarabu, utawala wa Israel umetangaza katika moja ya mitandao yake ya intaneti kuwa, "kitengo cha huduma za tiba katika jeshi la Israel kimetibu watu 2,600 wenye kubeba silaha ambao wamejeruhiwa vitani Syria tokea mwaka 2013 hadi sasa."
Hivi karibuni, Mohammad Badie, kinara wa wapinzani wa Syria waishio nje ya nchi amenukuliwa akimshukuru Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa hatua yake ya kuwatembelea magaidi katika hospitali za muda za utawala wa Kizayuni katika Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo.
Ripoti mbali mbali zimefichua uhusiano wa karibu uliopo baina ya utawala wa Israel na makundi ya magaidi wakufurishaji. Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Uangalizi wa Uwekaji Chini Silaha, UNDOF ambacho mwaka 1974 kilianza shughuli zake katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel hivi karibuni kilitoa ripoti maalumu katika Umoja wa Mataifa kuhusu ushirikiano wa moja kwa moja wa wanajeshi wa Israeli na magaidi walioko Syria wanaoungwa mkono na madola ya kigeni. Kadiri siku zinavyosonga mbele, inawabainikia walimwengu kuwa viongozi wa Syria wamekuwa wakisema kweli kuwa makundi ya kigaidi nchini humo yanapata misaada na kuungwa mkono na madola ya Magharibi na utawala wa Israel.
Nyaraka mbali mbali zinaonyesha kuwa vinara wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh wamekuwa na ushirikiano wa karibu na mashirika ya Ujasusi ya Marekani. Huo ni uthibitisho kuwa ISIS na makundi mengine ya kigaidi yameanzishwa kwa msaada wa kifedha wa Marekani na Saudia Arabia na hivi sasa yanatekeleza ukatili na fitina zao kwa usimamizi wa Israel na madola ya Kiarabu.
Makundi haya ya kigaidi yameanzishwa kwa ajili ya kuhudumia malengo ya madola ya Magharibi na Wazayuni na yanatenda kila aina ya jinai kufikia malengo hayo.Ukatili na uovu wa makundi ya magaidi unashabihiana sana na vitendo vya ukatili vya Wazayuni. Ni wazi kuwa utawala wa Kizayuni hutumia kila fursa ipatikanayo kuendeleza sera zake za kujitanua nchini Syria ili nchi hiyo iondoke katika duara la mrengo wa muqawama wa mapambano dhidi ya Wazayuni katika eneo.
Katika fremu hii, kufuatia kuibuka machafuko nchini Syria Machi 2011, utawala wa Kizayuni na madola ya Magharibi yalitumia vibaya maandamano ya baadhi ya wananchi na kwa njia hiyo wakapenyeza makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Utawala wa Kizayuni umeshadidisha uchokozi wa kijeshi dhidi ya Syria sambamba na kuibua fitina katika nchi hiyo ili serikali ya Damascus ishughulishwe na mgogoro wa ndani ya nchi na kushindwa kuwa kituo cha harakati za ukombozi wa Palestina kama ilivyokuwa kwa miongo kadhaa sasa. Hakuna shaka kuwa, nchi za eneo hasa Syria, inakabiliwa na tatizo kubwa la hujuma ya magaidi wa kigeni katika fremu ya njama hatari ya utawala wa Kizayuni, madola ya Magharibi na tawala waitifaki wao katika eneo.
Kwa mtazamo wa weledi wa mambo ya kisiasa, makundi ya kigaidi ambayo katika miaka ya hivi karibuni yameibuka katika eneo hasa nchini Syria na Iraq kama vile Al Qaeda, Jabhatu Nusra, ISIS na Ansaru Sharia hayangeweza kufika yalikofika pasina msaada wa maajinabi hasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Weledi wa mambo wanasema, utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya miongo sita sasa umekalia kwa mabavu ardhi za Palestina kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani na sasa pia kwa msaada wa Marekanina umeanzisha makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati ili kuzidhoofisha nchi za eneo na kwa njia hiyo kuzisahaulisha kadhia muhimu ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.