Marekani kutuma zana mpya za kivita nchini Syria
Marekani imeazimia kupeleka zana zake mpya za kivita nchini Syria sambamba na kutuma askari wengine 1,000 nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, kundi la wanamgambo wa Kikurdi walioko Syria wanaojulikana 'Kikosi cha Demokrasia Syria' (SDF) kimefichua kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inalenga kutuma askari wengine 1,000 katika nchi hiyo inayokumbwa na vita. Imedaiwa kuwa askari hao wa Marekani watahusika katika oparesheni za kuukomboa mji wa Raqqa unaokaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi la ISIS.
Afisa wa SDF ambaye hakutaka jina lika litajwe ameongeza kuwa, Marekani inatazamiwa kuingiza idadi kubwa ya silaha, vifaru, magari ya deraya, makombora, mizinga na zana nyinginezo katika eneo hilo la Syria.
Hayo yanajiri wakati ambao Rais Donald Trump wa Marekani wakati wa kampeni zake mwaka jana alimkosoa vikali rais wa wakati huo, Barack Obama kwa kuingilia kijeshi nchini Syria.
Tayari kuna wanajeshi zaidi ya 1,000 wa Marekani nchini Syria bila idhini ya serikali ya Damascus.
Hivi karibuni Rais Bashar Assad wa Syria alisema wanajeshi wote wa kigeni waliongia nchini humo bila idhini ya seirikali yake ni wavamizi.