Kamanda Qais Khazali: Marekani ndio inayowaingiza Madaesh Iraq
Katibu Mkuu wa Harakati ya ''Aswaib Ahlil-Haqq ya nchini Iraq, Qais Khazali amesema kuwa, Marekani ndio muhusika mkuu katika kuwaingiza wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh nchini humo.
Khazali ameyasema hayo kupitia mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Sumariyyah News ambapo sanjari na kuashiria njama za maadui za kuzusha moto wa fitina nchini Iraq, amesema Marekani ilianzisha kundi hilo la kigaidi kwa lengo la kuwasha moto huo wa fitina nchini humo. Ameongeza kuwa, licha ya wananchi wa Iraq kuishi katika maisha magumu na yasiyoridhisha kutokana na harakati za kigaidi na kadhalika mazingira mabaya ya kimaisha, lakini wako makini sana kuhusiana na njama za maadui. Katibu Mkuu wa Harakati ya ''Aswaib Ahlil-Haqq ya nchini Iraq, ameashiria pia juu ya nafasi ya chanya ya harakati za wananchi za kujitolea katika kukabiliana na wanachama wa kundi hilo na kusema, harakati hizo za kiraia zimeweza kufelisha mipango ya makumi ya miaka ya maadui wa Uislamu na Iraq kwa ujumla sanjari na kulirejeshea taifa hilo izza yake. Wakati huo huo Hadi al-Amiri, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Badr nchini Iraq ameisifu harakati ya kujitolea ya wananchi kwa kusema kuwa, harakati hiyo imekuwa muhimu sana ya kutegemewa kwa ajili ya ushiriki wa kuyakomboa maeneo yote yanayodhibitiwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Itafahamika kuwa, harakati hiyo ya wananchi kwa kushirikiana na jeshi la serikali, imeiletea mafanikio makubwa na ushindi wa kihistoria Iraq dhidi ya makundi ya kigaidi sanjari na kukwamisha kusonga mbele magaidi hao nchini humo.