Wapalestina wa Gaza wasusia kula kuwaunga mkono wafungwa wa Kipalestina
Wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza wamesusia kula chakula ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Kipalestina ambao wanadhalilishwa katika jela na magereza ya utawala haramu wa Israel.
Habari zinasema kuwa, wanachama 500 wa harakati ya muqawama ya Jihadi Islami wanaongoza kampeni hiyo ya kususia chakula tangu jana Alkhamisi, ili kuwaunga mkono wafungwa wa Kipalestina katika jela za kutisha za utawala huo wa Kizayuni, ambao wamesusia kula kwa takriban wiki mbili sasa.
Kadhalika wananchi wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wanatazamiwa kujiunga na wenzao katika kususia kula, huku shule, biashara na sekta ya uchukuzi zikifungwa katika eneo hilo kwa ajili ya mpango huo.
Kundi kubwa la waandamanaji limepiga kambi katika Medani ya Yasser Arafat katika mji wa Ramallah, baada ya kufanya maandamano katika barabara za Ukingo wa Magharibi, kuonyesha uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Kipalestina.
Mgomo wa kususia kula Wapalestina zaidi ya 1,500 wakiongozwa na Marwan Al-Barghuthi ambaye anatumikia kifungo cha maisha jela ulianza tarehe 17 Aprili kwa kaulimbiu ya "Uhuru na Heshima" katika magereza yote ya utawala wa Kizayuni.
Hali hii imeitiia wasiwasi Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ambapo juzi Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo alimuandikia barua Peter Maurer, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu akiitaka jumuiya hiyo iingilie kati na kukomesha ukandamizaji na mateso dhidi ya wafungwa wa Kipalestina katika jela za kutisha za utawala huo wa Kizayuni sambamba na kuwashurutisha watawala wa Israel kuangalia maslahi ya wafungwa waliosusia kula wa Kipalestina, kwa mujibu wa miongozo na viwango vya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.