Marekani: Mashambulizi yetu yameua mamia ya raia Iraq na Syria
Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, imetoa taarifa na kukiri kwamba mashambulizi ya muungano unaodaiwa kupambana na magaidi wa Daesh hadi sasa yameshaua raia 352 katika nchi za Iraq na Syria tangu mwaka 2014.
Shirika la habari la Reuters limeinukuu Wizara ya Ulinzi ya Marekani ikisema jana Jumapili kwamba, raia 45 wameuliwa kwenye mashambulizi hayo katika kipindi cha baina ya mwezi Novemba 2016 hadi Machi 2017 pekee. Kwa mujibu wa ripoti za Wamarekani wenyewe, wanajeshi wa Marekani wameua raia 26 wa Iraq na Syria katika kipindi cha mwezi wa Machi pekee.
Hata hivyo takwimu zinazotolewa na Marekani kuhusu raia wanaouliwa huko Iraq na Syria katika mashambulizi yanayoongozwa na nchi hiyo, ni ndogo mno ikilinganishwa na idadi kubwa ya raia wanaouawa kila leo.
Baadhi ya taasisi za uchunguzi wa matukio ya Iraq zinasema kuwa, zaidi ya raia 2500 wameuawa katika mashambulizi ya ndege za Marekani kwenye nchi za Iraq na Syria hadi hivi sasa.
Muungano unaodaiwa ni wa kupambana na magaidi wa Daesh ulianzishwa wakati wa Rais Barack Obama wa Marekani. Hata hivyo si tu mashambulizi ya muungano huo yameshindwa kuwamaliza magaidi hao, lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba raia wa kawaida ndio wahanga wakuu wa mashambulio hayo. Muungano huo unaundwa na nchi ambazo zinahesabiwa ni waungaji mkono wakuu wa kifedha na kisilaha wa magenge ya kigaidi likiwemo Daesh.