Umoja wa Mataifa na hali ya haki za binadamu nchini Bahrain
Duru ya 27 ya kikao cha Umoja wa Mataifa kimeanza mjini Geneva kwa lengo la kuchunguza hali ya haki za binadamu nchini Bahrain.
Nchi washiriki wa kikao hicho, juzi walianza kuchunguza faili la haki za binadamu la utawala wa Bahrain kwa kuuuliza utawala huo maswali 39. Kwa mujibu wa tangazo la timu ya Umoja wa Mataifa ambayo ni amilifu katika uwanja wa kuchunguza haki za binadamu nchini Bahrain ni kuwa, nchi 91 zimetaka kufanyike uingiliaji kati na uchunguzi kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Bahrain.
Asasi za kitaifa na kimataifa zimetangaza kuwa, hali ya haki za binadamu nchini Bahrain katika miaka ya 2012 hadi 2017 ni mbaya mno hasa kutokana na kuweko kesi kama za kupokonywa uraia, kubaidishwa kwa lazima, kuzuiwa kusafiri, kupigwa marufuku wanasheria kushiriki katika kikao cha haki za binadamu cha Umoja wa Mataifa na kuzuiwa watu kushiriki katika mikusanyiko ya amani sambamba na hatua ya utawala wa Manama ya kuwatesa raia.
Hivi sasa wasiwasi wa kimataifa kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini Bahrain umekuwa ukiongezeka kila siku na kufanyika vikao mbalimbali vya kimataifa vya kuchunguza hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo ni jambo linalounga mkono nukta hii. Katika mazingira kama haya, utawala wa Aal Khalifa ukiwa na lengo la kuzuia kufichuliwa zaidi jinai zake katika asasi za kimataifa daima umekuwa ukizuia kuweko wanaharakati wa Bahrain katika asasi za kisheria. Katika uwanja huo, daima viongozi wa Bahrain wamekuwa wakifanya kila wawezalo ili kuhakikisha kwamba, wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu wa nchi hiyo hawashiriki katika vikao vya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva kwa ajili ya kuchunguza hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu dhidi ya ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi. Utawala huo ukiwa na lengo la kuzima sauti na cheche za moto wa malalamiko hayo umewatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa, vijana na raia wengi wa nchi hiyo na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela. Natija ya siasa hizo za utumiaji mabavu za utawala wa Aal Khalifa zimeifanya Bahrain kuwa uwanja wa ukandamizaji na mbinyo dhidi ya raia. Fauka ya hayo, watawala hao wamekwenda mbali zaidi na kuwapokonya uraia baadhi ya wanaharakati na wapinzani wa nchi hiyo.
Hatua hiyo ya serikali ya Manama ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa. Katika kipengee cha 15 tangazo la kimataifa la haki za binadamu imeelezwa wazi kuwa, watu wote wana haki ya kunufaika na uraia na kwamba, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kujichukulia maaamuzi na kumnyima mwenzake haki ya uraia.
Kwa hakika utawala wa Bahrain umekuwa ukitumia kila wenzo ili kukabiliana na harakati za upinzani dhidi yake na hata hatua ya kuwapokonya uraia wapinzani inalenga kuwafuta katika ulingo wa siasa za nchi hiyo. Katika mazingira kama haya, kuendelea kigugumizi cha Umoja wa Mataifa na kusitasita kwake kuuchukulia hatua utawala wa Bahrain ni jambo lisilokubaliwa hata kidogo na fikra za waliowengi ulimwenguni; kwani hali hiyo itaufanya utawala huo uendelee na ukandamizaji na ukiukaji wake wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wa Bahrain bila ya wasiwasi wowote.