May 03, 2017 03:45 UTC
  • Magaidi wa ISIS washambulia kambi ya wakimbizi Syria na kuua 36

Kwa akali watu 36 wameuawa katika shambulizi la kigaidi dhidi ya kambi ya wakimbizi lililofanywa jana Jumanne na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, kaskazini mashariki mwa Syria.

Shirikia linalojiita Syrian Observatory for Human Rights limesema magaidi watano wa kujitolea muhanga wa Daesh walijiripua katika kambi hiyo iliyoko mjini Rajm al-Salibeh, katika mkoa wa kaskazini mashariki wa Hasakah, karibu na mpaka wa Syria na Iraq. 

Habari zinasema kuwa, kambi hiyo ilikuwa na wakimbizi raia wa Iraq na raia wachache wa Syria ambao wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na kushadidi vita na machafuko nchini humo.

Kambi ya wakimbizi nchini Syria yenye raia wa Iraq

Rami Abdel Rahman, Mkuu wa Syrian Observatory for Human Rights amesema zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo ya kigaidi aghalabu yao wakiwa na majeraha ya risasi walizofyatuliwa na magaidi hao wa Daesh kabla ya kujiripua.

Haya yanajiri masaa machache baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani kutoa taarifa na kukiri kwamba mashambulizi ya muungano unaodaiwa kupambana na magaidi wa Daesh hadi sasa yameshaua raia 352 katika nchi za Iraq na Syria tangu mwaka 2014, wakiwemo raia 26 wa Iraq na Syria katika kipindi cha mwezi wa Machi pekee.

 

Tags