Idadi ya waliouawa shahidi katika shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria yaongezeka
Idadi ya watu waliouawa shahidi katika shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria imeongezeka na kufikia watu 14.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika rasmi la Habari la Syria (SANA), watu 14 wameuawa shahidi na wengine 43 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni jana usiku kutokea kaskazini-magharibi mwa Lebanon dhidi ya ngome za kijeshi katika eneo la katikati ya Syria.
Hapo kabla, Yasal Haider, mkurugenzi wa hospitali ya mji wa Misyaf iliyoko katika viunga vya magharibi mwa mkoa wa Hama, Syria, alitangaza kuwa raia wanne waliuawa shahidi na wengine 14 walijeruhiwa katika shambulio hilo la kinyama la anga la Wazayuni katika eneo hilo, na kwamba hali za baadhi yao ni mbaya.
Kwa upande mwingine, mtandao wa Al-Mayadeen umetangaza katika ripoti yake kwamba; shambulio la utawala katili wa Israel limelenga kituo cha utafiti wa kisayansi na mitambo ya majaribio ya kiulinzi katika viunga vya mji wa Misyaf.
Katika miaka ya hivi karibuni, mashambulizi yaliyofanywa mara kadhaa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Damascus na maeneo mengine tofauti ya Syria, yamekuwa mara nyingi yakizimwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo.