Mtoto Mpalestina auawa shahidi Gaza katika hujuma ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2905-mtoto_mpalestina_auawa_shahidi_gaza_katika_hujuma_ya_israel
Mtoto Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 10 ameuawa shahidi katika hujuma mpya ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 12, 2016 08:16 UTC
  • Mtoto Mpalestina auawa shahidi Gaza katika hujuma ya Israel

Mtoto Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 10 ameuawa shahidi katika hujuma mpya ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Yasin Abu Hussa alipoteza maisha wakati ndege za kivita za Israel zilipovamia mji wa Beit Lahiya kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza mapema leo Jumamosi.

Dada yake mtoto huyo, Isra, mwenye umri wa miaka sita naye amepata majeraha mabaya kichwani huku ndugu yake, Ayoub, mwenye umri wa miaka 13 naye pia akipata majeraha madogo.

Hivi karibuni harakati za Kiislamu na kitaifa za Palestina zimetahadharidha kuhusu hali mbaya ya watu wa eneo la Ukanda wa Gaza kutokana na mzingiro wa kidhalimu wa utawala haramu wa Israel dhidi ya eneo hilo.

Harakati za kupigania uhuru wa Palestina za Hamas, Jihad Islami, Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Palestina na Harakati ya Kidemokrasia zilitoa taarifa zikisema kuwa, hali mbaya ya watu wa Ghaza ni matokeo ya kuendelea mzingiro na hujuma za Israel dhidi ya watu wa eneo hilo, migawanyiko na hitilafu za ndani na kwamba mzingiro huo umezidisha umaskini, ukosefu wa ajira na mgogoro mkubwa.

Mwezi Januari Benki ya Dunia ilitoa taarifa ikitahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya uhaba wa chakula unaolikabili eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Tahadhari hiyo ya Benki ya Dunia imeeleza kwamba, Ukanda wa Gaza unakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na eneo hilo kuendelea kusumbuliwa na mzingiro wa miaka 10 wa utawala wa Kizayuni wa Israel.