Bahrain inazidi kuwakandamiza wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i2965-bahrain_inazidi_kuwakandamiza_wapinzani
Shirika moja la kutetea haki za binadamu Bahrain limeutuhumu utawala wa kifalme nchini humo kuwa umezidisha ukandamizaji na utesaji wapinzani wa kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2016 03:50 UTC
  • Bahrain inazidi kuwakandamiza wapinzani

Shirika moja la kutetea haki za binadamu Bahrain limeutuhumu utawala wa kifalme nchini humo kuwa umezidisha ukandamizaji na utesaji wapinzani wa kisiasa.

Jukwaa la Haki za Binadamu Bahrain limetoa ripoti Jumamosi na kuashiria ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi kati ya Machi 3 na Machi 11 mwaka huu.

Ripoti hiyo imesema katika kipindi hicho , vikosi vya Bahrain vimewakamata na kuwaweka kizuizini watu 13 huku kukiripotiwa kesi tisa za utesaji.

Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussein, kwa mara nyingine tena alilaani ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain na kusema kuwa, serikali ya Manama imedhihirisha namna isivyoheshimu haki za wapinzani nchini humo.

Kadhalika afisa huyo wa UN alivitaka vyombo vya mahakama kukomesha tabia ya kutoa hukumu zisizo za kiadilifu dhidi ya raia wa nchi hiyo na haswa hukumu ya kuwapokonya uraia wananchi wake wanaoonekana kuukosoa utawala huo wa kifalme.

Tangu mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa malalamiko ya wananchi dhidi ya siasa za utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa. Mauaji, ukandamizaji na utiaji nguvuni watu yamekuwa ndio maelekezo makuu yanayotekelezwa muda wote na vikosi vya polisi ya utawala huo wa kifamilia.