Jun 02, 2017 13:30 UTC
  • Nafasi ya kipekee ya Saudia katika kuenea fikra za Kiwahabi duniani

Abdul Malik al Houthi, Katibu Mkuu wa harakati ya Answarullah ya Yemen ametangaza kuwa, nchi ambayo hivi sasa inaongoza fikra za Kiwahabi na kuzieneza katika nchi mbalimbali duniani, ni Saudi Arabia.

Ikumbukwe kuwa fikra ya Kiwahabi ndiyo inayoeneza vitendo vya kigaidi katika maeneo tofauti ulimwenguni na ndicho chanzo cha ukosefu wa amani katika nchi za Pakistan, Afghanistan, barani Afrika, eneo la magharibi mwa Asia yaani Mashariki ya Kati na katika miji tofauti ya barani Ulaya. 

Vile vile Abdul Malik al Houthi alisema Jumatano usiku katika hotuba aliyoitoa kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwamba, uhusiano wa karibu sana uliopo baina ya Marekani na Saudi Arabia ndio uliomfanya rais wa Marekani Donald Trump aichague Riyadh kuwa sehemu yake ya kwanza kuitembelea nje ya Marekani tangu atangazwe kuwa rais wa nchi hiyo na unaonesha nchi hizo mbili zinashirikiana katika kuenea vitendo hivyo vya kigaidi.

Kwa kweli viongozi wa Saudi Arabia wanadai kuwa wanapambana na ugaidi katika hali ambayo wao ndio waungaji mkono wakubwa wa fikra zinazozalisha vitendo vya kigaidi duniani kwa kushirikiana na Marekani ambayo viongozi wake kama Donald Trump, wanashindwa hata kuficha uadui wao kwa Waislamu. Tunapovitupia jicho vitendo vya Saudi Arabia ndani na nje ya nchi hiyo tutaona kuwa, magaidi wengi wa eneo la magharibi mwa Asia na duniani kiujumla imma wana asili ya Saudia au wameathiriwa na fikra za Kiwahabi za Saudi Arabia na wanapata uungaji mkono wa kifedha na kisilaha kutoka kwa ukoo wa Aal Saud.

Hii ni katika hali ambayo, Marekani kwa upande wake inajali tu maslahi yake hivyo inashirikiana na Saudi Arabia kustafidi kadiri inavyoweza na vitendo vya magenge ya kigaidi kwa ajili ya kueneza fitna katika safu za Waislamu na kufunika nafasi ya Saudia katika vitendo vya kigaidi vya magenge hayo.

Ukweli ni kuwa, chanzo cha kifikra cha kanali nyingi za kigaidi na kitakfiri ni misimamo mikali iliyopotoka ya Kiwahabi. Fikra hizo potofu zina nafasi muhimu katika kuzuka vitendo vya kigaidi na fitna za Aal Saud kwenye eneo hili na duniani kiujumla.

Mfalme wa Saudi Arabia akimpa mkono mke wa rais wa Marekani

Moja ya vitendo vya ukoo wa Aal Saud ni kuzusha wimbi la mizozo ya kimadhehebu duniani na kuzusha mifarakano popote pale wanapoona Waislamu wametulia na wanaishi kwa salama na amani. Wanatumia fikra za Kiwahabi kuwaita Waislamu wengine washirikina, makafiri na watu wa bidaa na hivyo kuwatoa katika Uislamu kwa mambo madogomadogo na kuwashughulisha na mambo yasiyo ya kimsingi ili kuwaweka mbali na umoja na mshikamano wao. 

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, chanzo cha Uwahabi ni wakoloni wa Uingereza waliozianzisha na kuzitia nguvu fikra hizo ili kuipaka matope dini tukufu ya Kiislamu. Leo hii wakoloni na madola ya kibeberu duniani yanafanya juhudi kubwa za kutumia fikra za Kiwahabi na vitendo vya kigaidi na vya kikatili kufunika mafundisho sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu ambayo ni dini ya amani, ubinadamu na iliyojaa mapenzi na kuishi na watu kwa utulivu na usalama. Kuenea vitendo vya kikatili, misimamo mikali na ukosefu wa amani duniani ni matunda ya siasa za Aal Saud za kueneza fikra ya Kiwahabi kwa baraka kamili za Marekani. Matunda ya fikra za Kiwahabi ni magenge ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh (ISIS) ambayo hayajali chochote bali yanafanya jinai kubwa katika miji tofauti ya Ulaya, Asia, Afrika bali hata huko Marekani kwenyewe kwa jina la Uislamu. 

Kwa kweli fikra ya Kiwahabi haiishii tu ndani ya Saudi Arabia au katika eneo la magharibi mwa Asia, bali ina wafuasi katika kila kona ya dunia. Mchango wa Saudia katika kuzuka makundi ya kitakfiri na kigaidi na kuenea fikra hizo katika maeneo mbalimbali duniani kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani ambazo ndizo zilizoansisha fikra hizo na kuzitia nguvu, ni mkubwa. Leo hii uhakika huu uko wazi kwa kila mtu kwamba, utawala wa Aal Saud ambayo ni chimbuko la fikra za Kiwahabi na chanzo cha makundi ya kigaidi katika maeneo taofauti duniani, kuanzia Afghanistan hadi Marekani, una nafasi kuu katika ukosefu wa amani duniani. Kutiwa mbaroni mamia ya magaidi raia wa Saudi Arabia katika nchi za Syria, Iraq, Yemen, Marekani na katika nchi mbalimbali za Ulaya, ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo.

Tags