Marekani ndiye muhusika mkuu wa vita vya Yemen
Katibu Mkuu wa harakati ya Answarullah ya nchini Yemen amesisistiza kuwa, Marekani ndiye muhusika mkuu wa mashambulizi na uvamizi wa Yemen ambao unatekelezwa na Saudi Arabia na Imarati.
Televisheni ya al Masirah ya nchini Yemen imemnukuu Abdul Malik Badruddin al Houthi akisema hayo jana usiku katika hotuba aliyoitoa mjini Sana'a na kuongeza kuwa, wavamizi wa Yemen wametenda jinai katika mikoa yote ya nchi hiyo, hivyo ameyataka makundi yote ya Yemen kusimama imara kukabiliana na wavamizi wa nchi yao.
Amesema, wavamizi hao wanafanya njama za kutumia vibaya matatizo mbalimbali waliyoisababishia Yemen lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu njama zao zote zitafeli.

Katibu Mkuu wa harakati ya Answarullah amesema, mamluki na vibaraka wa madola ya kigeni hawana nafasi yoyote nchini Yemen.
Badruddin al Houthi ameashiria namna utawala wa Kizayuni wa Israel ulivyo na manufaa ya pamoja na ukoo wa Aal Saud katika uvamizi wa Yemen na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa nao uko pamoja na wavamizi hao.
Tarehe 26 Machi 2015, Saudi Arabia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na kwa baraka kamili za Marekani na utawala wa Kizayuni zilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Yemen. Hata hivyo hadi hivi sasa wavamizi hao wameshindwa kufikia malengo yao ghairi ya kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu, kuua kwa umati mamia ya raia Waislamu wa nchi hiyo na kuwafanya wakimbizi makumi ya maelfu ya wengine.