Qatar: Madai dhidi yetu si ya kweli na hayana msingi
Baada ya Saudi Arabia, Misri, Imarati na Bahrain kukata uhusiano na Qatar mapema leo Jumatatu, wizara ya mambo ya nje wa Qatar imesema, imesikitishwa na hatua hiyo.
Televisheni ya Al Alam imenukulu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ikisema leo kuwa, hatua hiyo ya kukata uhusiano haiwezi kutetewa na imechukuliwa kwa kutegemea madai ya urongo na yasiyo na msingi.
Taarifa hiyo imesema hatua hiyo ya kukata uhusiano haitakuwa na taathira katika maisha ya raia wa nchi hizo nne nchini Qatar.
Aidha Qatar imesema, itachukua hatua za kusambaratisha njama zenye lengo la kuathiri vibaya uchumi wa raia wa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.
Mapema leo Jumatatu, nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati, Bahrain na Misri zimekata uhusiano wao wa kidiplomasia na mahusiano yote ya majini na angani na Qatar zikiituhumu nchi hiyo kuwa inaunga mkono ugaidi na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo.