UN yalaani Israel kuwazimia umeme Wapalestina Ghaza
Umoja wa Mataifa umelaani hatua ya utawala haramu wa Israel kuwazimia kwa muda mrefu umeme Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Katika taarifa Jumatano, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Robert Pipe amesema, "kuongezwa muda wa kukatwa umeme kunaweza kupelekea kuporomoka huduma zote za kimsingi hasa huduma za afya na maji."
Tahadhari hiyo imekuja siku tatu baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutangaza mpango wa kupunguza zaidi kiwango cha umeme unaopelekwa Ghaza kwa karibu dakika sitini kwa siku. Hivi sasa eneo hilo lenye wakaazi milioni 1.84 hupokea umeme kwa takribani masaa matatu pekee kwa siku.
Utawala haramu wa Israel umedai umechukua hatua hiyo baada ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina iliyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kupunguza kwa asilimia 30 malipo yake ya umeme wa Ghaza.
Weledi wa mambo wanasema uamuzi huo wa mamlaka hiyo inayoongozwa na Mahmoud Abbas ni njia ya kuishinikiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ili iondoke madarakani Ghaza. Hamas imekuwa ikitawala Ghaza tokea mwaka 2007 baada ya kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia na tokea wakati huo eneo hilo limekuwa chini ya mzingiro wa kinyama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani.
Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa.