HAMAS: Uhusiano wetu na Iran ni imara
Kiongozi mmoja muhimu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa harakati hiyo daima itaendelea kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada yake kwa taifa la Palestina bila ya kutarajia malipo yoyote kutoka kwao.
Leo Jumatano, shirika la habari la Tasnim limemnukuu Mahmoud al Zahar, mmoja wa viongozi wakubwa wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS akiashiria uhusiano madhubuti na makini uliopo baina ya harakati hiyo na Tehran na kusema kuwa, Iran ambayo ni sehemu muhimu ya umma wa Kiislamu inatoa misaada mingi kwa taifa la Palestina na bila ya kudai chochote kutoka kwao.
Al Zahar ameashiria pia ripoti zisizo na msingi na zisizo sahihi za baadhi ya vyombo vya habari zinazodai kuwa serikali ya Doha imewataka viongozi wa HAMAS waondoke nchini Qatar na kusema kuwa, lengo la kusambazwa habari hizo za uongo ni kujaribu kuchafua sura ya HAMAS.
Mjumbe huyo mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palesitna HAMAS aidha amegusia namna alivyopandwa na hasira Adel al Jubeir, waziri wa mambo ya nje wa Saudia kutokana na uungaji mkono wa Qatar kwa harakati ya HAMAS na kusema kuwa, lengo la Saudi Arabia ni kueneza fitna na uchochezi katika umma wa Kiislamu na kumfurahisha rais wa Marekani, Donald Trump.