Hamas yataka Israel ishinikizwe ili iheshimu haki za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31446-hamas_yataka_israel_ishinikizwe_ili_iheshimu_haki_za_wapalestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa mwito wa kubanwa na kushinikizwa utawala haramu wa Israel ili uheshimu haki za wananchi madhulumu wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 07, 2017 03:19 UTC
  • Hamas yataka Israel ishinikizwe ili iheshimu haki za Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa mwito wa kubanwa na kushinikizwa utawala haramu wa Israel ili uheshimu haki za wananchi madhulumu wa Palestina.

Mwito huo umetolewa na Hazem Kassem, msemaji Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ambaye amesisitiza kwamba, kuna haja kwa nchi mbalimbali ulimwenguni kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel ili uchunge na kuheshimu haki za Wapalestina.

Hazem Kassem amezitaka nchi zote na jamii ya kimataifa kukata uhusiano wao na utawala huo vamizi ambao umekuwa ukitenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi wa Palestina.

Aidha afisa huyo wa ngazi za juu wa Hamas amepokea kwa mikono miwili na kusifu matokeo ya kikao cha hivi karibuni cha chama tawala nchini Afrika Kusini ANC kilichoitaka serikali ya nchi hiyo kupunguza kiwango cha uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel.

Nembo ya chama tawala nchini Afrika Kusini ANC

Itakumbukwa kuwa, katika mkutano wa siku ya Jumatano wa kamati ya sera ya chama cha ANC uliofanyika mjini Johannesburg, chama hicho kilisisitiza kushikamana kwake na taifa la Palestina na kuitaka serikali ipunguze kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia na Israel ikiwa ni katika fremu ya malengo na misingi ya chama hicho ya kupigani ukombozi.

Hivi karibuni Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisisitiza kuwa, nchi yake inaunga mkono suala la kuasisiwa nchi huru ya Palestina ili kuhitimisha mzozo wa Mashariki ya Kati.