Israel yazidisha uchokozi wa kijeshi dhidi ya Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3361-israel_yazidisha_uchokozi_wa_kijeshi_dhidi_ya_lebanon
Baada ya kufichuka awamu mpya ya ujasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon, mbunge mmoja wa nchi hiyo amesema hatua ya Wazayuni kujipenyeza katika laini za mawasiliano ya Lebanon ni hujuma kwa usalama na mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo na ametaka hatua zichukuliwe kukabiliana hali hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 19, 2016 07:37 UTC
  • Israel yazidisha uchokozi wa kijeshi dhidi ya Lebanon

Baada ya kufichuka awamu mpya ya ujasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon, mbunge mmoja wa nchi hiyo amesema hatua ya Wazayuni kujipenyeza katika laini za mawasiliano ya Lebanon ni hujuma kwa usalama na mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo na ametaka hatua zichukuliwe kukabiliana hali hiyo.

Hassan Fadlallah, mwenyekiti wa kamati ya mawasiliano katika Bunge la Lebanon ameashiria kufichuliwa mtandao mpya ujasusi wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika laini za mawasiliano ya simu katika maeneo ya mpakani kusini mwa Lebanon na kusema, jamii ya kimataifa inapaswa kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kuihujumu Lebanon kijasusi.

Mkuu wa kamati ya mawasiliano katika Bunge la Lebanon ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umeweka mtandao maalumu wa kusikiliza mazungumzo ya simu na kufanya ujasusi katika eneo lote la mpaka wa Lebanon na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawla huo. Amebaini kuwa Wazayuni wanafuatilia kila aina ya harakati iwe ya kijeshi au isiyo ya kijeshi katika eneo hilo, jambo ambalo amesema ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Mwezi uliopita, Radio ya Utawala wa Kizayuni ilinukulu duru za kijeshi na kiusalama za utawala huo zikisema kuwa, baada ya kuwekwa mfumo wa kisasa wa kijasusi ndani ya ardhi ya Lebanon, jeshi la Israel linaweza kupata habari za kisiri katika eneo hilo.

Kufichuliwa mitandao kadhaa ya kijasusi ya Israel kusini mwa Lebanon katika kipindi cha mwaka moja uliopita kunajiri katika hali ambayo karibu kila siku jeshi la Israel hukiuka mipaka ya Lebanon ya angani, nchi kavu na baharini hatua ambazo zinaenda kinyume cha azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lilihitimisha vita vya siku 33 vya mwaka 2006 vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon. Pamoja na kuwepo azimio hilo utawala wa Kizayuni unaendeleza hatua za uhasama dhidi ya Lebanon.

Duru za usalama Lebanon zinadokeza kuwa, utawala wa Kizayuni baada ya kushindwa katika vita hivyo vya siku 33 ulianzisha vita vya kijasusi dhidi ya Harakati ya Hizbullah.

Kwa mujibu wa ripoti za kila mwaka za vyombo vya sheria vya Lebanon, katika kipindi cha miaka sita iliyopita zaidi ya washukiwa 100 wamekamatwa wakifanyia ujasusi shirika la kijasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad.

Kwa msingi huo siku ya Jumamosi, Harakati ya Hizbullah na Mrengo wa Mustakbal ambayo ni makundi mawili makuu ya kisiasa Lebanon yalisisitiza kuhusu kukabiliana na na njama za adui Mazayuni na kumchukulia hatua kali kila ambaye anatishia usalama wa nchi hiyo.

Chokochoko mpya za jeshi la utawala wa Kizayuni katika mapaka wa kusini mwa Lebanon zinajiri huku Lebanon ikipitia kipindi kigumu cha mgogoro wa kisiasa na kiusalama kutokana na harakati za makundi ya kigaidi, kuwepo pengo la utawala baada ya wabunge kushindwa kumchagua rais sambamba na maandamano ya wananchi wanakosoa utendaji mbovu wa serikali.

Kwa hivyo vyama vya kisiasa Lebanon vimeonya kuhusu kuendelea hali ya hivi sasa na kusisitiza kuwa kuchaguliwa rais mpya n njia bora zaidi ya kuiondoa nchi hiyo katika dimbi la matatizo ya ndani na kupunguza hatari ya makundi ya kigaidi na uhasama wa Wazayuni dhidi ya nchi hiyo.