Mahujaji wa Nyumba ya Allah watoa ujumbe amani kwa walimwengu wote
-
Amir wa mji mtakatifu wa Makkah, Khalid al Faisal
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Amir wa Makkah akisema kuwa, mwaka huu zaidi ya mahujaji milioni mbili wameshiriki katika ibada za jangwa la Arafa na hao ni wawakilishi wa Waislamu zaidi ya bilioni moja na milioni 800 ambao wamewafikishia walimwengu wote ujumbe wa amani na kuishi pamoja kwa usalama.
Shirika hilo la habari limemnukuu Khalid al Faisal, Amir wa Makka akiwaambia waandishi wa habari leo Jumatatu kuwa, vyombo vya kuwasiliana na umma navyo vina wajibu wa kueneza na kuwafikishia walimwengu wote ujumbe huo wa usalama na amani wa mahujaji.
Ameongeza kuwa, msimu wa Hija unahusiana tu na ibada na hauhusiani na masuala mengine kama kile kinachoitwa utalii wa kidini.
Amir huyo wa Makkah aidha ameelezea matumaini yake kwamba Waislamu watafanya juhudi kubwa zaidi za kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu kukabiliana na baadhi ya watu ambao wanaipaka matope dini hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Juzi Jumamosi pia, Amir huyo wa Makkah, alisema kuwa mahujaji wa Iran ni "ndugu zetu wa kidini" na aliwaombea kheri, baraka na amani.
Televisheni ya al Alam ilitangaza habari hiyo na kumnukuu Amir huyo wa Makkah akisema mbele ya waandishi wa habari kwamba "mahujaji wa Iran ni ndugu zetu wa kidini na tunawakaribisha katika ardhi takatifu za Saudi Arabia."