Sep 24, 2017 03:32 UTC
  • Iran: Historia haitasahau jinai zinazofanywa na Saudia huko Yemen

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa historia ya dunia haitasahau jinai na uhalifu mkubwa unaofanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen.

Abbas Araqchi ameyasema hayo katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliofanyika mjini New York huko Marekani na kusisitiza kuwa, historia haiwezi kusahau uhalifu na jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya wanawake, watoto na watu wa Yemen kwa ujumla. 

Maiti za watoto waliouawa na Saudi Arabia huko Yemen

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ametilia mkazo udharura wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu na kusema kuwa: Jumuiya ya OIC ndiyo sehemu inayofaa zaidi kwa ajili ya kudhihirisha umoja huo. 

Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Kenneth Roth amekemea kimya cha Umoja wa Mataifa mbele ya jinai zinazoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen. Amesema Wayemeni wanaendelea kuuawa kila siku katika mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake na kwamba nchi hiyo kwa sasa inasumbuliwa na njaa. 

Watu wa Yemen wanakufa kwa njaa kutokana na mzingiro wa Saudia na washirika wake

Zaidi ya watu elfu 13 wa Yemen wameuawa kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudia na washirika wake. 

Tags