Palestina yakubaliwa kuwa mwanachama wa Interpol
Palestina imekubaliwa kuwa mwanachama kamili wa Polisi ya Kimataifa (Interpol), katika hatua inayoonekana ni pigo la kidiplomasia kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani.
Palestina pamoja na Kisiwa cha Solomon zimepewa uanachama huo hii leo katika Kongamano Kuu la Interpol lililofanyika katika mji mkuu wa China, Beijing.
Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imeandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, asilimia 75 ya wanachama wa shirika hilo kuu la polisi imepiga kura kuunga mkono kupewa uanachama Palestina.
Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina amesema ushindi huo kwa Wapalestina umetokana na irada thabiti ya Interpol kutaka kupambana na jinai na kuhakikisha kuwa sheria hazikiukwi katika sehemu yoyote ile duniani.
Jitihada za Palestina za kutaka kujumuishwa kuwa mwanachama wa Interpol ziligonga mwamba mwaka jana, hatua ambayo ilipongezwa na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu na watawala wa Marekani.
Novemba mwaka 2012, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura na kuinyanyua Palestina kutoka 'Taasisi Tazamaji' hadi 'Taifa Tazamaji', hatua ambayo ilipelekea taifa hilo la Kiarabu kupata uanachama wa mashirika mbali mbali ya kimataifa, kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO.