Mchakato wa mapatano ya kitaifa ya Wapalestina na vitisho vinavyowakabili
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35357-mchakato_wa_mapatano_ya_kitaifa_ya_wapalestina_na_vitisho_vinavyowakabili
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetahadharisha kuhusu mipango ya kimataifa ya kutaka kutumiwa vibaya mapatano ya kitaifa ya Wapalestina lengo likiwa ni kufutilia mbali kadhia ya Palestina.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 07, 2017 23:09 UTC
  • Mchakato wa mapatano ya kitaifa ya Wapalestina na vitisho vinavyowakabili

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetahadharisha kuhusu mipango ya kimataifa ya kutaka kutumiwa vibaya mapatano ya kitaifa ya Wapalestina lengo likiwa ni kufutilia mbali kadhia ya Palestina.

Khalid al Batsh, afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina juzi alikaribisha hatua za harakati za Fat-h na Hamas za kufikia mapatano ya kitaifa na kumaliza hitilafu za ndani ili kupunguza mateso na masaibu ya wananchi wa Palestina na hivyo kuweza kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni.  

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Jihadul Islami aliyasema hayo katika maandamano makubwa yaliyofanywa juzi Ijumaa na raia wa Palestina katika mji wa Ghaza. Al Batsh ameongeza kuwa Wapalestina hawapaswi kuziruhusu pande za kimataifa kuvuruga kadhia ya Palestina kwa kisingizio cha mapatano ya kitaifa na kukanyaga haki na misingi ya kitaifa ya Wapalestina. Aidha ametilia mkazo kufikiwa mapatano hayo kwa mujibu wa stratijia ya kitaifa ili kukabiliana ipasavyo na adui Mzayuni. 

Khalid al Batsh, Afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina 

Makundi ya muqawama ya Palestina siku zote yanasisitizia  udharura wa kuendelezwa mapambano na jihadi dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni na kupinga kupokonywa silaha makundi ya muqawama hadi kung'olewa utawala huo dhalimu. 

Duru mpya ya mapatano ya kitaifa ya Wapalestina katika wiki za hivi karibuni imedhihirisha wazi mikakati yake ya wazi kuhusu ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Wapalestina katika kusimamia masuala yao na pia kuandaa na kufuatilia ramani ya njia kwa minajili ya kufanikisha malengo ya Palestina. Aidha matukio chanya yaliyojitokeza katika uga wa kisiasa wa Palestina hayajaufurahisha utawala wa Kizayuni na waitifaki wake hususan Marekani. Katika mazingira hayo, pande hizo zinafanya kila ziwezalo na kutumia njia mbalimbali kuzuia kufikiwa mapatano ya kitaifa ya Wapalestina na hivyo kuyasitisha au kuyatoa katika mkondo wake wa asili  na kisha kuyatumia kama ngazi ya kufanikisha mwenendo eti wa mapatano ya mashariki.

Ni kutokana na njama zote hizo ndio maana makundi ya Palestina yakatahadharisha kuhusu vitisho vikuu vinavyoyakabili mapatano hayo ya Wapalestina. Hii ni katika hali ambayo, vitisho hivyo vyote havijaishia hapo, bali katika wiki za hivi karibuni Wapalestina walikabiliwa na wimbi kubwa la makelele na tuhuma za Marekani. Tuhuma hizo za  Marekani kwa makundi ya muqawama ya Palestina na hatua ya nchi hiyo ya kuyataja makundi hayo kuwa ni ya kigaidi, zinaweza kutathminiwa kuwa ni siasa za kipropaganda za upotoshaji na uhasama za viongozi wa Washington. Hatua zote hizo za Marekani kwa mara nyingine tena zimeweka wazi uadui wa viongozi wa Marekani kwa wananchi wa Palestina na njama zao za kutaka kuzuia kikamilifu  kupatikana haki za wananchi wa Palestina. Matukio hayo ya Palestina yanatoa udharura wa kuwa macho zaidi wananchi wa Palestina na upuuzaji wowote katika uwanja huo utakuwa na madhara hatari kwa Wapalestina. Kufikiwa mapatano kati ya Wapalestina kutaimarisha muqawama wao mbele ya njama za utawala wa Kizayuni na Marekani; na kutaandaa uwanja wa kupatikana haki za raia wa Palestina ikiwemo kuundwa nchi ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds.