Oct 08, 2017 02:41 UTC
  • Amnesty yailaani UN kwa kujaribu kudunisha jinai za Saudia nchini Yemen

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limeulaani Umoja wa Mataifa kwa kujaribu kudunisha jinai za muungano wa Saudi Arabia dhidi ya watoto wa Yemen katika vita dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Siku ya Alhamisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwasilisha ripoti ya kila mwaka kuhusu Watoto na Migogoro ya Kivita ambapo Saudia imewekwa katika orodha nyeusi kutokana na jinai zake za kuwaua na kuwajeruhi watoto wa Yemen.

Mwaka jana Saudia ilifanikiwa kuzuia kuwekwa jina lake katika orodha hiyo wakati katibu mkuu wa wakati huo wa Umoja huo Ban Ki-moon aliposhinikizwa kuondoa jina la Saudia.

Mwaka huu pamoja na kuwa Saudia na waitifaki wake katika muungano wa vita dhidi ya Yemen wamewekwa katika orodha ya Umoja wa Mataifa ya nchi zinazoua watoto vitani, lakini umoja huo umedai kuwa eti muungano huo umechukua hatua za kuwalinda watoto vitani. Ibara hiyo imeongezwa ili kuzuia Saudia kukemewa kimataifa.

Uharibifu unaosababishwa na ndege za kivita za Saudia katika maeneo ya raia nchini Yemen

Amnensty International imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Mataifa ya kudai eti Saudia imechukua hatua za kuwalinda watoto vitani. Sherine Tadros wa Amnesty International amesema kila mara wakati Umoja wa Mataifa unapolegeza msimamo na kuwaruhusu watenda jinai kukwepa ukosoaji  au kufikishwa katika vyombo vya mahakama, jambo hilo huwapa kiburi cha kutenda jinai zaidi. Amnesty imesema ni aibu kwa Umoja wa Mataifa kusalimu amri mbele ya mashinikizo. Ripoti ya UN imesema mwaka 2016 Saudia ilihusika katika vifyo vya watoto 683 nchini Yemen na kwamba ilishambulia shule na mahospitali 38 katika nchi hiyo.

 

Tags