Hamas: Hakuna wa kutushurutisha tuvunje jeshi letu au tuitambue Israel
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema hakuna mtu mwenye uwezo wa kuishurutisha harakati hiyo ya muqawama kuvunja tawi lake la kijeshi au kuutambua utawala haramu wa Israel kama masharti ya kukubali mapatano ya kitaifa ya Wapalestina.
Yahya Sinwar, kiongozi mpya wa Hamas aliyasema hayo jana Alkhamisi, kama radiamali yake kwa masharti hayo yaliyotolewa na Marekani ili iyakubali mapatano hayo.
Amesema "Hakuna yeyote duniani mwenye uwezo wa kutupokonya silaha. Kinyume chake, tutaendelea kuwa na nguvu za kuwalinda wananchi wetu. Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kutulazimisha kutambua ukaliaji wa mabavu wa ardhi zetu."
Wakati huo huo, Ezat al-Rashaq, mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amesema kuwa mapatano ya kitaifa ya Palestina yameutia woga na wasiwasi utawala wa Kizayuni na kubainisha kuwa, jibu zuri zaidi kwa masharti hayo ya Israel ni kuendeleza harakati kwa nguvu zote ili kuimarisha umoja miongoni mwa Wapalestina.
Naye Fauz Barhum, Msemaji wa Harakati ya Muqawama ya Hamas pia amesisitiza kuwa masharti yaliyotolewa na utawala wa Kizayuni na Marekani ili zikubali mapatano ya kitaifa ya Palestina ni uingiliaji wa masuala ya Palestina usiokubalika na kwamba masharti hayo yanapasa kujibiwa baada ya kufikiwa mapatano hayo.
Siku chache zilizopita, Hamas ilitangaza kufikia mapatano ya maelewano ya kitaifa na chama cha Fat'h chini ya upatanishi wa Misri, kwa lengo la kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa muongo mmoja kuhusu utawala wa Ukanda wa Gaza.