Amnesty, HRW zalaani hukumu dhidi ya familia ya mwanaharakati wa Bahrain
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yamekosoa vikali hatua ya mahakama moja ya Bahrain ya kutoa hukumu zisizo za kiuadilifu dhidi ya watu watatu wa familia ya mwanaharakati mashuhuri wa nchi hiyo anayeishi nje ya nchi.
Samah Hadid, Mkurugenzi wa Kampeni wa Amnesty International mjini Beirut amesema kutolewa hukumu dhidi ya watu wa familia ya Sayed Ahmed Alwadaei, kufutia mchakato usio wa kiuadilifu wa kesi ni katika njama za serikali ya Manama za kumuadhibu kwa njia isiyo ya moja kwa moja mwanaharakati huyo mashuhuri.
Naye Joe Stork, Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kuhukumiwa vifungo watu wa familia ya Sayed Alwadaei ni ithibati tosha kuwa utawala wa Bahrain upo tayari kutumia kila njia kuwanyamazisha wapinzani na wakosoaji wake.
Utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain umekuwa ukiwatia mbaroni na kuwazuilia wanaharakati wa nchi hiyo, wanaoonekana kuukosoa utawala huo. Mwezi Juni mwaka huu, utawala wa Aal-Khalifa ulimfutia uraia Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri na mkuu wa kimaanawi wa mapinduzi ya watu wa nchi hiyo suala ambalo lilikabiliwa na radiamali kali kutoka ndani na nje ya nchi hiyo.
Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya al-Wifaaq nchini Bahrain ni shakhsia mwingine ambaye amekuwa akizuiliwa na vyombo vya sheria vya Aal-Khalifa tangu mwezi Julai mwaka jana kwa tuhuma bandia dhidi yake.
Bahrain imekumbwa na malalamiko na maandamano ya amani ya wananchi tangu Februari 14 mwaka 2011. Takwa kuu la wananchi wa Bahrain kwa utawala ulioko madarakani ni kuwa wanataka kuwepo madarakani serikali halali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, kukomeshwa ubaguzi, kufanyika marekebisho ya kisiasa, kuheshimiwa haki za binadamu, kutekelezwa uadilifu na uhuru na kuacha kuwa na utegemezi kwa nchi za Magharibi.