Indhari ya Lebanon kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36871-indhari_ya_lebanon_kwa_jumuiya_ya_nchi_za_kiarabu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon ameamwandikia barua Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) akimwambia kwamba, umoja huo unapaswa kufungamana na makubaliano ya Waarabu ambayo yalitofautisha baina ya muqawama na ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 27, 2017 10:18 UTC
  • Indhari ya Lebanon kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon ameamwandikia barua Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) akimwambia kwamba, umoja huo unapaswa kufungamana na makubaliano ya Waarabu ambayo yalitofautisha baina ya muqawama na ugaidi.

Gebran Bassil ametahadharisha katika barua yake hiyo kwa Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo ni jibu kwa taarifa ya hivi karibuni ya jumuiya hiyo iliyoitaja harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwamba ni kundi la kigaidi kuwa, kuzusha anga ya ukosefu wa amani na utulivu nchini Lebanon kutakuwa na taathira hasi kwa nchi za Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon amesema kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zinataka kudhoofisha muqawama na mapambano ya Lebanon mbele ya ugaidi na utawala haramu wa Israel. Njama hizo zinafanyika katika hali ambayo, muqawama na mapambano ya wananchi wa Lebanon ni misdaqi na kielelezo cha wazi cha "Haki ya Kisheria ya Kujihami". Kujihami na kujilinda ni haki ya kisheria  ambayo imeashiriwa katika kipengee cha 51 cha hati ya Umoja wa Mataifa na ni haki ya kisheria ambayo imetumiwa na Lebanon kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi.

Moja ya mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League)

Katika fremu hiyo, Harakati ya Hizbullah ikiwa moja ya nguzo za kiulinzi katika Mashariki ya Kati imekuwa na ushiriki mzuri na amilifu katika medani ya siasa za Lebanon. Kuegemea Lebanon kwa jeshi na muqawama wa wananchi unaoongozwa na Hizbullah kumepelekea kusambaratishwa njama dhidi ya nchi hiyo na hatua hiyo imeifanya Lebanon kuwa ngome imara mkabala na hatua za kibeberu na za kuzusha fitinz  za Israel, magaidi wa kitakfiri pamoja na waungaji mkono wao katika Mashariki ya Kati. Huu ni ukweli ambao umeutia kiwewe utawala ghasibu wa Israel na watawala wa Kiarabu wanaounga mkono ugaidi katika eneo hili.

Hali hii imeifanya Lebanon hususan harakati ya Hizbullah iandamwe na wimbi la njama za kila upande kutoka kwa maadui wa nchi hiyo yaani Israel, Saudi Arabia na madola ya Magharibi hususan Marekani. Hii leo ugaidi unatumiwa kama wenzo na tawala za Kiarabu kwa ajili ya kukandamiza makundi ya kiraia na ya kisiasa ya ndani ya nchi zao.

Ahmad Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuuiya ya Nchi za Kiarabu

Tukitupia jicho matukio ya miongo ya huko nyuma tunaona kuwa, ulimwengu wa Kiarabu uliwasaliti wananchi wa mataifa hayo hususan malengo matukufu ya Wapalestina na Walebanon na ukawa pamoja na Marekani na Israel, hali ambayo iliufanya uwe nyuma ya pazia ya njama dhidi ya muqawama na mapambano ya nchi mbili hizo na eneo la Mashariki ya Kati kwa ujumla.

Matokeo ya hayo yamekuwa kwa namna ambayo, Israel ambayo kuna siku ilikuwa ikitamani kuwa na uhusiano na nchi za Kiarabu na hivyo iondoke katika hali ya kutengwa, hivi sasa imepata jeuri na kufikia hatua ya kuzitaka nchi za Kiarabu ziiweke Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi kama sharti la kuanzisha uhusiano na nchi hizo.

Ni katika fremu hiyo ndio maana hivi karibuni Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambalo linaundwa na nchi za Kiarabu za ukanda wa Ghuba ya Uajemi liliiweka Hizbullah katika orodha ya makundi ya kigaidi kutokana na maelekezo ya Saudia. Hii ni katika hali ambayo, madola makubwa ya Kimagharibi yenye kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati nayo yamo katika harakati za kuendesha propaganda chafu dhidi ya muqawama na mapambano ya wananchi.

Hizbullah ya Lebanon

Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana tunaona kuwa, kila mara makundi na harakati za wananchi zinapopata ushindi dhidi ya ugaidi katika Mashariki ya Kati, muungano eti wa kupambana na ugaidi unaoongozwa na Marekani huingia uwanjani na kufanya njama za kuonyesha kwamba, mafanikio hayo si lolote si chochote.

Muungano huo sambamba na kuharibu haiba na sura ya muqawama na kuutaja kuwa ni ugaidi, umekuwa ukifanya njama za kupotosha ukweli wa mambo na wakati huo huo kujionyesha kwamba, wenyewe ndio mpambanaji wa kweli dhidi ya ugaidi. Ili kukabiliana na anga kama hii, viongozi mbalimbali wa eneo hili wamekuwa wakisisitiza udharura wa kutofautishwa baina ya muqawama na ugaidi. Barua ya indhari ya Gebran Bassil, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon  kwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana na fitina za jumuiya hiyo, inabainisha wazi kupoteza hadhi na itibari jumuiya hiyo mbele ya macho ya nchi za eneo hili.