Lebanon yazitaka nchi za Kiarabu ziiwekee Marekani vikwazo
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Lebanon amezitaka nchi za Kiarabu ziiwekee Marekani vikwazo vya kiuchumi kutokana na hatua ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.
Akiongea katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Cairo, Misri hapo jana, Gebran Bassil amesema kitendo hicho cha Trump kinapaswa kukabiliwa na vikwazo vya pande zote dhidi ya Marekani.
Amesema nchi wanachama wa Arab League zinafaa kuichukulia Marekani hatua za kidiplomasia, kisiasa na kisha vikwazo vya kiuchumi na kifedha.
Bassil amesema anatumai mgogoro huo ulioibuliwa na Trump utaziamsha kutoka usingizini nchi za Kiarabu na kuzileta pamoja, akisisitiza kuwa iwapo zitaifumbia macho kadhia hiyo, basi historia haitawasamehe.
Kwa upande wake, Ahmed Aboul-Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ameuambia mkutano huo kuwa, kuna udharura wa mataifa yote duniani kulitambua taifa huru la Palestina, mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu.
Naye Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mambo wa Nje wa Palestina amezitaka nchi wanachama wa Arab League ziwaagize wajumbe wao katika Umoja wa Mataifa kuwasilisha kwa Baraza la Usalama la umoja huo, rasimu ya azimio la kukabili hatua hiyo ya kichokozi ya Trump, inayoendelea kulaaniwa katika kila kona ya dunia.