Jumuiya ya NAM yakosoa hatua ya Marekani dhidi ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37559-jumuiya_ya_nam_yakosoa_hatua_ya_marekani_dhidi_ya_quds
Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) imekosoa vikali hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitambua Quds kuwa eti mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 13, 2017 15:25 UTC
  • Jumuiya ya NAM yakosoa hatua ya Marekani dhidi ya Quds

Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) imekosoa vikali hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitambua Quds kuwa eti mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika mkutano uliofanyika Paris, Ufaransa chini ya uenyekiti wa Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, nchi wanachama wa jumuiya hiyo wamekitaja kitendo hicho cha Trump kuwa kinyume cha sheria na kinachokinzana na sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

NAM imesema mpango wowote wa kubadilisha hali ya Quds na asasi au nchi yeyote ni kinyume cha sheria na hatua ambayo haina itibari.

Kadhalika nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote kwa pamoja zimeafikiana kwamba, tangazo hilo la Trump dhidi ya Quds ni uamuzi wa upande mmoja unaokiuka makubaliano ya kimataifa kuhusu hali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu hususan mji wa Quds (Jerusalem).

Tangazo la Trump dhidi ya Quds limelaaniwa katika kila kona ya dunia 

Disemba 6, Trump alitangaza kuwa Washington imeutambua rasmi mji wa Baitul Muqaddas au Quds kama mji mkuu wa utawala wa Israel na kuagiza kuanza mchakato wa kuuhamishia ubalozi wake mjini huko kutoka Tel Aviv, licha ya hatua hiyo kukabiliwa na upinzani mkubwa kieneo na kimataifa.

Uamuzi huo wa Trump umekabiliwa na wimbi la malalamiko katika pembe mbalimbali duaniani hususan katika nchi za Kiislamu na Kiarabu.