Mabunge ya nchi za Kiislamu yatakiwa kuingilia kadhia ya Palestina
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ameyataka mabunge ya nchi za Kiislamu kuingia kadhia ya Quds na Palestina ili kukabiliana na njama za Marekani za kutaka kuwapora Waislamu Kibla chao cha Kwanza.
Kazem Jalali amesema hayo alipohojiwa na shirika la habari la Bunge la Iran na kuongeza kuwa, baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kudhihirisha wazi uadui wake dhidi ya Waislamu na kutangaza kuitambua Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu utawala wa Kizayuni wa Israel, asasi mbalimbali za nchi za dunia zimeonyesha radiamali yao kali dhidi ya uadui huo, hivyo wakati umefika kwa mabunge ya nchi za Kiislamu nayo kuingia moja kwa moja kwenye suala hilo.
Mbunge huyo mwandamizi wa Iran aidha amegusia maandamano ya Waislamu milioni mbili na nusu wa Indonesia yaliyofanyika siku ya Jumatatu kumlaani Donald Trump na kubainisha kuwa, mataifa ya Kiislamu yako macho uwanjani na yamesimama imara kulihami taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Amma kuhusiana na tarehe ya kufanyika kikao cha kila mwaka cha Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu, Jalali amesema, kikao hicho kinatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao wa Januari 2018 hapa mjini Tehran. Kikao hicho kinatarajiwa kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi nyingi na ndani yake kutafanyika vikao tanzu kikiwemo cha kamati ya Palestina ya Umoja wa Mabunge ya Kiislamu.
Tarehe 6 mwezi huu wa Disemba, rais wa Marekani aliitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel na hapo hapo akatoa amri ya kufanyika taratibu za kuuhamishia mjini humo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala dhalimu wa Kizayuni.