Wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37931-wasiwasi_kuhusu_ukiukwaji_wa_haki_za_binadamu_nchini_bahrain
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limebainisha wasiwasi wake kuhusu kuendelea ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bahrain na kusema, jambo hilo linaashiria kuwa utawala wa Aal Khalifa unalenga kuzima sauti za wapinzani katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2017 03:48 UTC
  • Wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bahrain

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limebainisha wasiwasi wake kuhusu kuendelea ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bahrain na kusema, jambo hilo linaashiria kuwa utawala wa Aal Khalifa unalenga kuzima sauti za wapinzani katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Katika taarifa yake shirika la Amnesty Internation limesema utawala wa kifalme nchini Bahrain unakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na kutaja mfano wa kufunguliwa mashtaka mapya kiongozi wa chama cha upinzani cha Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al Wefaq, Sheikh Ali Salman. Aidha mifano mingine imetajwa kuwa ni kubatilishwa usajili wa Jumuiya ya Kitaifa ya Demokrasia ya Kivitendo (Wa'ad) na pia kupelekwa katika mahakama ya kijeshi mtetezi wa haki za binadamu Nabeel Rajab.

Amnesty International imesema kesi hizo ni sehemu ya kampeni ya watawala wa Bahrain ya kukandamiza wapinzani hata wale wanaoishi nje ya nchi.

Askari wa Bahrain wakizima maandamano ya wapizani

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, licha ya Bahrain kuwa nchi ndogo zaidi katika eneo la Magharibi ya Asia lakini ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu wake. Na hii ni katika hali ambayo, utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa ungali unaendeleza siasa zake za ukandamizaji kwa uungaji mkono wa madola ya Magharibi.

Tangu Februari 14, 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopigania uhuru na uadilifu na kutaka nchi hiyo iongozwe na utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe; lakini mauaji, hatua kali za ukandamizaji na hata kuwavua uraia wananchi ndilo jibu ambalo utawala wa kifalme wa Aal Khalifa umekuwa ukitoa mbele ya matakwa halali ya wananchi hao. Itakumbukwa kuwa, Saudi Arabia imetuma jeshi nchini Bahrain kukandamiza wananchi.