Sheikh Nabil Qaouk: Kuiunga mkono Beitul-Muqaddas ni jukumu la Hizbullah
Mjumbe wa Baraza Kuu la Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, kuiunga mkono Beitul-Muqaddas ni jukumu la harakati hiyo na kwamba, Hizbullah itaendelea kubakia mstari wa mbele katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.
Sheikh Nabil Qaouk amesema kuwa, umma wa Kiarabu na Kiislamu umegawanyika katika mihimili miwili ambapo kundi la kwanza limeiacha na kuitelekeza Palestina na kundi la pili likiliunga mkono taifa madhulumu la Palestina.
Sheikh Nabil Qaouk ameongeza kuwa, Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon kwa hali yoyote ile haitaacha kuiunga mkono Palestina.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon amebainisha kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel unajifakharisha wazi kwamba, radiamali ndogo kabisa kuhusiana na uamuzi wa Rais Donald Trump wa kuitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel ilitoka kwa Saudi Arabia.
Amebainisha kuwa, Saudia Arabia ni nchi iliyofanya jinai kubwa zaidi na kuitishia zaidi jamii ya mwanadamu katika mwaka huu 2017 unaoelekea ukingoni.
Amesema, Saudia imefanya mzingiro dhidi ya wananchi wa Yemen, mauaji na jinai na kuwafanya raia milioni 15 wa nchi hiyo kuwa katika hali mbaya ya kibinadamu.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, Saudi Arabia ndio kikwazo kikuu cha nguvu na umoja wa Waarabu katika kuiunga mkono na kuihami Beitul-Muqaddas na Palestina kwa ujumla.