Shakhsia wa kisiasa wa Palestina: Intifadha inaendelea
Viongozi kadhaa wa kisiasa wa Palestina wametangaza kuwa Intifadha ya Wapalestina itaendelea hadi utakapofutwa uamuzi uliotangazwa na rais wa Marekani wa kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Viongozi hao wametangaza msimamo huo katika kongamano la "Quds, Mji Mkuu wa Milele wa Palestina" lililoitishwa na harakati ya Jihadul Islami katika mji wa Gaza na kutoa wito wa kuwepo umoja wa kitaifa na ushirikishaji wa kisiasa sambamba na kuundwa jeshi la kitaifa kwa ajili ya kulinda matukufu ya ardhi ya Palestina.
Aidha wamesisitizia ulazima wa kusimamishwa ushirikiano na uratibu wa pamoja wa kiusalama uliopo baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni.
Mahmoud Az-Zahar, kiongozi mwandamizi wa harakati ya Hamas ameliambia kongamano hilo kwamba: walowezi wa Kizayuni watahasirika mno kwa kuivamia ardhi ya Palestina na akasisitiza kwamba: Wapalestina hawatoyauza katu matukufu yao kwa ajili ya kupatiwa pesa.

Sheikh Nafidh Azzam, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Jihadul Islami, amesema: uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuitambua rasmi Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ni sawa na kukiuka sheria za kimataifa na akasisitiza kwamba Marekani inafanya kila njia kulinda usalama wa Israel; nao Wapalestina wanazitaka nchi za Kiarabu ziangalie upya uhusiano wao na Marekani.
Kasisi Manuel Musallam, kiongozi wa kiroho wa Wakristo wa Palestina na mjumbe wa Kamati ya Kiislamu na Kikristo ya Kuyahami Matukufu ya Palestina amewataka walimwengu wasikubali eneo la Mashariki ya Kati lisukumwe kwenye vita vya kidini. Amesisitiza kuwa heshima na izza ya Waislamu na Waarabu imefungamana na Quds na kwamba kukaliwa kwa mabavu Quds kutawafanya Waarabu wawe duni na dhalili.

Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Desemba, Rais Donald Trump wa Marekani aliamsha hasira za walimwengu kwa kutangaza kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel na kuagiza zichukuliwe hatua za maandalizi ya kuuhamishia katika mji huo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv.
Hatua hiyo ya Trump imekabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya Palestina na katika maeneo mbalimbali ya dunia.../