Assad: Njama za adui za kuigawa Syria zimegonga mwamba
Rais wa Syria ameeleza kuwa ushindi wa jeshi la nchi hiyo umepelekea kuandaliwa njia ya kurejesha amani nchini humo.
Akizungumza huko Damascus na Alexander Lavrentiev Mjumbe Maalumu wa Rais Vladimir Putin wa Russia katika masuala ya Syria, Rais Bashar al Assad wa Syria ameeleza kuwa ushindi muhimu uliopata jeshi la Syria, Russia na waitifaki wake wengine katika kuusambaratisha ugaidi umepelekea kufeli njama za adui za kutaka kuigawa Syria na eneo hili kwa ujumla.
Rais Assad amesisitiza kuwa nchi za Magharibi kwa muda sasa zimeshiriki katika njama ya kuigawa Syria. Naye Alexander Lavrentiev ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Syria ametilia mkazo uungaji mkono wa Moscow kwa mchakato wa mapambano dhidi ya ugaidi huko Syria.

Lavrentiev ameongeza kuwa Russia itatoa misaada yote inayohitajika ili kuisadia serikali na wananchi wa Syria kulinda umoja wa kitaifa wa nchi hiyo. Pande mbili hizo zimechunguza pia masuala mbalimbali yakiwemo mazungumzo yajayo ya Syria yatakayofanyika katika mji wa Suchi nchini Russia na mchakato wa mazungumzo kati ya serikali ya Syria na wapinzani.