Vita vya kidini; mbinu mpya ya Wazayuni ya kuidhibiti Beitul-Muqaddas
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i40993-vita_vya_kidini_mbinu_mpya_ya_wazayuni_ya_kuidhibiti_beitul_muqaddas
Katika kuendeleza vita vyake vya kila upande dhidi ya taifa madhulumu la Palestina, mara hii utawala wa Kizayuni wa Israel umekuja na mbinu mpya ambapo kwa kuongeza kodi ya misikiti na maeneo matakatifu ya kidini ya Waislamu na Wakristo umeshadidisha vita vya kidini dhidi ya taifa la Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2018 01:05 UTC

Katika kuendeleza vita vyake vya kila upande dhidi ya taifa madhulumu la Palestina, mara hii utawala wa Kizayuni wa Israel umekuja na mbinu mpya ambapo kwa kuongeza kodi ya misikiti na maeneo matakatifu ya kidini ya Waislamu na Wakristo umeshadidisha vita vya kidini dhidi ya taifa la Palestina.

Hatua hiyo ya Israel imekabiliwa na upinzani mkali wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ambayo imetangaza katika taarifa yake kwamba: Hatua ya Israel ya kuongeza kodi ya misikiti na maeneo matakatifu ya kidini ya Waislamu na Wakristo na kuweka vizingiti vya kuingia katika maeneo hayo imekuwa kizuizi kwa Wapalestina kuingia katika maeneo hayo kwa ajili ya kutekeleza faradhi za kidini. Sehemu moja ya taarifa hiyo ya HAMAS imesema:

Utawala wa Kizayuni wa Israel umechukua hatua hatari kabisa ya kuyalenga matukufu ya Wapalestina hivyo kuna haja ya kusimama kidete na kukabiliana na hatua hiyo. Kuyatwisha kodi maeneo ya kihistoria na kidini ya Quds pamoja na miliki zake ni matokeo ya hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Beitul-Muqaddas. Sisi tunasisitiza juu ya kupanuliwa Intifadha ya Quds dhidi ya wavamizi sambamba na kukabiliana na mipango na malengo ya utwala haramu wa Israel dhidi ya Palestina.

Muonekano wa mji wa Beitul-Muqaddas

Hapana shaka kuwa, hatua za serikali ya Marekani na utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina katu haziwezi kufanikiwa kupotosha ukweli wa kihistoria wa taifa la Palestina na wala hatua hizo kamwe haziwezi kuhalalisha uvamizi wa Israel dhidi ya Beitul-Muqaddas. Ulimwengu wa Kiislamu na fikra za waliowengi ulimwenguni zina yakini kwamba, Quds kubwa utabakia kuwa mji mkuu wa milele na wa daima wa ardhi ya kihistoria ya Palestina. Aidha mipaka ya asili ya Palestina itachorwa kwa mapambano halali ya kupigania ukombozi, muqawama na damu za Wapalestina.

Kwa hakika hatua zilizo dhidi ya dini za utawala vamizi wa Israel dhidi ya taifa la Palestina zimeshadidi kiasi kwamba, zimeifanya hata Mamlaka ya Ndani ya Palestina kupaza sauiti ya malalamiko. Yusuf al-Mahmoud, msemaji serikali ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Kuchukua kodi kutoka katika nyumba za ibada kama misikiti na makanisa, ni uvamizi mpya wenye uchochezi mpya ambao unaulenga mji wa Beitul-Muqaddas, umma wa Kiarabu na Kiislamu hususan Wapalestina na kuyacheza shere matukufu yao.

Kwa hakika kuyalenga maeneo ya kidini na nyumba za ibada ni ukiukaji wa wazi wa nyaraka na makubaliano yote ya kimataifa ambayo yanadhamini uhuru wa kuabudu na ambayo yanaheshimu nafasi ya maeneo matakatifu ya kidini katika mazingira yoyote na mahala popote. Historia inaonyesha kuwa, tangu kale wananchi wa Palestina walikuwa wakiishi katika ardhi hizo za mababu zao na siku zote wamekuwa wakifungamana na misingi kama ya huba, udugu, ushirikiano, heshima kwa wengine na kuzitukuza dini za mbinguni. Bila shaka kufungwa maeneo matakatifu ya kidini, kunazijeruhi hisia za Wapalestina. Hatua hiyo mbaya haikubaliki na bila shaka wananchi wa Palestina katu hawatakubaliana na jambo hilo.

Khalid Mash'al

Khalid Mash'al, Mkuu wa zamani wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amezikosoa vikali baadhi ya pande katika Mashariki ya Kati ambazo zipo pamoja na mipango ambayo lengo lake ni kuifuta kadhia ya Palestina na kushadidishwa hujuma na mashambulio dhidi ya Beitul-Muqaddas.

Mash'al anasema kuwa, laiti kusingekuweko vibaraka wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Donald Trump asingethubutu kuutangaza mji wa Baitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Aidha amesema kuwa, uamuzi wa Marekani wa kuuhamishia huko Baitul-Muqaddas ubalozi wake hapo Mei 14 mwaka huu ni mwendelezo wa jinai na kuzichochea hisia za Wapalestina; kwani tarehe hiyo inakumbusha tukio chungu la kukaliwa kwa mabavu Palestina mnamo mwaka 1948.