Kushindwa huko Yemen, majanga ya makamanda wa jeshi la Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i41149-kushindwa_huko_yemen_majanga_ya_makamanda_wa_jeshi_la_saudi_arabia
Mabadiliko ya ghafla yaliyofanywa na Mfalme Salman katika serikali na jeshi la Saudi Arabia yametajwa na wachambuzi wengi wa kimataifa kuwa ni matokeo ya kushindwa na kukata tamaa katika vita vya nchi hiyo dhidi ya Yemen.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 04, 2018 03:54 UTC

Mabadiliko ya ghafla yaliyofanywa na Mfalme Salman katika serikali na jeshi la Saudi Arabia yametajwa na wachambuzi wengi wa kimataifa kuwa ni matokeo ya kushindwa na kukata tamaa katika vita vya nchi hiyo dhidi ya Yemen.

Maagizo ya kufutwa kazi maafisa wa ngazi za juu katika serikali na jeshi la Saudi Arabia yametolewa na Mfalme Salman kwa matakwa ya Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia. Mabadiliko haya yanatajwa kuwa huwenda ndiyo makubwa zaidi katika serikali ya Saudia na yamewasomba maafisa kadhaa wa ngazi za juu akiwemo Jenerali Abdul Rahman bin Saleh al-Bunyan aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Saudia na makamanda wa vikosi vya nchi kavu na anga. Sambamba na fagio hilo la chuma, Mfalme wa Saudi Arabia amewateua baadhi ya watu wa familia ya kifalme kushika nafasi na nyadhifa za jeshi la nchi hiyo. Inaonekana kuwa lengo la hatua hiyo ni kuwasimika watu waaminifu kwa familia ya kifalme na kutafuta uungaji mkono wa baadhi ya mirengo inayowania madaraka katika nchi hiyo ya kifalme. Mtandao wa habari wa Washington Post umechambua hatua ya hivi karibuni ya Muhammad bin Salman na mabadiliko yaliyopewa jina la "Mtikisiko wa Kitiba" na kuandika kuwa: Mabadiliko yaliyofanyika katika serikali ya Saudi Arabia ni mtikisiko wa kitiba wa dharura kwa ajili ya kusasisha maisha ya kiutamaduni na kisiasa ya Saudia. Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia amri na dikrii zilizotolewa na Mfalme zilizofanya mabadiliko makubwa katika jeshi na urasimu wa serikali ya Riyadh. Katika mabadiliko hayo pia mwanamke ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi.." 

Muhammad bin Salman

Kushindwa kwa jeshi la Saudi Arabia nchini Yemen pia kumewalazimisha watawala wa Riyadh kufanya mabadiliko ya dharura katika jeshi la nchi hiyo. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, miongoni mwa malengo makuu ya mageuzi hayo ni kumtayarishia njia nzuri zaidi mrithi kijana wa ufalme wa nchi hiyo na kuwaweka madarakani watu walioko karibu naye. Mabadiliko hayo yanakusudia kumdhihirisha Muhammad bin Salman kama mtu wa mageuzi, wa kisasa na mwenye mipango kabambe!

Ripota wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar anasema: Mageuzi yaliyofanyika Saudi Arabia ni kifuniko tu kinachoficha masuala yanayofanyika nyuma ya pazia. Baadhi ya masuala na maamuzi hayo ni yale yanayochukuliwa na kutolewa nyakati za usiku yakihusiana na jeshi la nchi hiyo. Inaonekana pia kwamba lengo la mageuzi haya ni kupata uungaji mkono wa baadhi ya mirengo inayokinzana ndani ya kizazi cha Aal Saud kupitia njia ya kuwapa vyeo na mamkala vinara wa mirengo hiyo. Maamuzi hayo yanachukuliwa kumsawazishia njia Muhammad bin Salman hata kama yatakuwa na madhara kwa jeshi la taifa. Safari ya kwanza kabisa iliyopangwa kufanywa na mrithi huyo kijana wa kiti cha ufalme katika nchi ya Kiarabu imepingwa na maafisa wengi wa ngazi za juu. Bin Salman pia ameshindwa katika vita vya Yemen na sasa jumuiya za kimataifa zinamtaja kuwa ni mtenda jinai na uhalifu wa kivita. Vilevile amezusha mgawanyiko katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi, na Saudi Arabia kwa sasa inapitia kipindi kigumu sana kutokana na sera na misimamo yake.

Donald Trump na Bin Salman

Bin Salman anajitayarisha kurithi nafasi ya baba yake na kuwa mfalme wa Saudi Arabia. Hata hivyo inaonekana kuwa, hatua ya kwanza ya kufikia kiti cha ufalme ni kuondoa majeshi ya nchi hiyo huko Yemen. Hivyo Muhammad bin Salman ambaye ndiye muhandishi wa mashambulizi na vita vya Yemen, ametambua kwamba hawezi kupata ushindi na sasa anataka kuwatupia lawama za vita hivyo makamanda wa ngazi za juu wa jeshi na kujivua yeye na aibu na fedheha hiyo. Hii ni pamoja na kuwa, Saudi Arabia inatumia kiwango kikubwa sana cha bajeti yake kwa ajili ya jeshi la nchi hiyo na kwa mujibu wa jarida la Forbes la Marekani, bajeti ya jeshi la nchi hiyo mwaka uliopita ilikuwa kubwa zaidi ya gharama za masuala ya kijeshi za Iran, Algeria, Iraq, Oman na Israel kwa pamoja. 

Pamoja na hayo wataalamu wa masuala ya kisiasa na kijeshi wanasema kuwa, jeshi la Saudi Arabia limedhalilishwa nchini Yemen mkabala wa wapiganaji wa harakati ya Ansarullah na sasa limeachwa nyuma hata na waitifaki wake huko Yemen kama Imarati.