Jumuiya ya Madaktari wa Kiarabu yatahadharisha kuhusu maafa ya kibinadamu Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i41743-jumuiya_ya_madaktari_wa_kiarabu_yatahadharisha_kuhusu_maafa_ya_kibinadamu_yemen
Jumuiya ya Madaktari wa Kiarabu imetahadharisha kwamba, msimu wa joto wenye maafa unawasubiri wananchi wa Yemen ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 16, 2018 14:25 UTC
  • Jumuiya ya Madaktari wa Kiarabu yatahadharisha kuhusu maafa ya kibinadamu Yemen

Jumuiya ya Madaktari wa Kiarabu imetahadharisha kwamba, msimu wa joto wenye maafa unawasubiri wananchi wa Yemen ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.

Abdul-Qawi al-Shamiri, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madkatari wa Kiarabu amesema kuuwa, hali ya kiafya nchini Yemen imekuwa ikizidi kuwa mbaya siku baada ya siku na kwamba, wananchi wa nchi hiyo wanahitajia msaada wa haraka.

Kuhusiana na misaada ya jumuiya hiyo, Abdul-Qawi al-Shamiri  amesema kuwa, hadi sasa jumuiya yao imetekeleza mipango ya awamu tano katika kuwasaidia wananchi hao.

Hivi karibuni, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) lilitahadharisha kwamba, hali ya ukosefu wa usalama wa chakula inazidi kuwa mbaya huko nchini Yemen.

Watoto wa Yemen wamekuwa wakiaga dunia kila siku kwa kukosa huduma za afya na tiba

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, Wayemeni milioni 22 na laki mbili wanahitajia misaada ya chakula na kwamba milioni 8 na laki nne miongoni mwao wanakaribia kukumbwa na baa la njaa.

Saudi Arabia ambayo inaungwa mkono kikamilifu na Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kisha kuiweka nchi hiyo chini ya mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani.

Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi tangu Saudia iivamie kijeshi nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Miundombinu ya Yemen pia imeharibiwa vibaya kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia.