Mchango wa Trump katika mauaji ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43702-mchango_wa_trump_katika_mauaji_ya_wapalestina
Wapalestina wasiopungua 94 wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala ghasibu wa Israel tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipoutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 27, 2018 01:44 UTC
  • Mchango wa Trump katika mauaji ya Wapalestina

Wapalestina wasiopungua 94 wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala ghasibu wa Israel tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipoutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Tarehe 6 Disemba mwaka jana Rais wa Marekani aliutambua rasmi mji wa Quds (Jerusalem) kuwa ni mjii mkuu wa Israel na akaamuru ubalozi wa nchi yake uhamishiwe katika mji huo licha ya upinzani mkubwa wa kimataifa. 

Tunapotazama matukio yaliyojiri Palestina baada ya Trump kushika madaraka ya kuiongoza Marekani tunaona kuwa, ukatili na mauaji ya Israel dhidi ya watu wa Palestina yameshika kasi zaidi kutokana na sera zisizo na mantiki za kiongozi huyo na uungaji mkono wa pande zote wa serikali ya Washington kwa Wazayuni maghasibu. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndiyo maana walimwengu wanaitambua Marekani kuwa ni mshirika wa Israel katika mauaji yanayofanywa dhidi ya raia wasio na hatia yoyote wa Palestina. 

Trump na Netanyahu

Naibu Mweyekiti wa Chama cha Saadan nchini Uturuki Hassan Bitamaz anasema: Hatua iliyochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani imeutia kiburi na jeuri zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel katika ukandamizaji wake huko Palestina. Vilevile Alauddin Borujerdi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Bunge la Iran amesema kuwa, Marekani ndiye mtuhumiwa nambari moja wa mauaji na jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina. Wakati huo huo Hannana Ashrawi ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina, (PLO) amesema kuwa, uamuzi wa Marekani kuhusu mji mtakatifu wa Quds umeitayarishia Israel uwanja wa kutekeleza jinai zaidi dhidi ya Wapalestina. Amesema Israel inataka kuufanya mji huo mtakatifu kuwa wa Kizayuni kikamilifu.

Hannana Ashrawi

Ushahidi unaonesha kuwa, Donald Trump ndiye anayezidi kuutia kiburi utawala haramu wa Israel kwani kama si himaya na uungaji mkono wake wa pande zote, Tel Aviv isingethubutu kufanya jinai na mauaji hayo. Tangu aliposhika madaraka ya Marekani, Trump amekuwa akichochea zaidi migogoro ya kikanda na kimataifa kutokana na sera na siasa zake zisizo na mantiki. Wachambuzi wa mambo wanasema lengo la hatua ya Trump ya kuiarifisha Israel kama dola la Kiyahudi ni kuua kikamilifu uwezekano wa kuundwa nchi huru ya Palestina mji wake mkuu ukiwa Quds tukufu. Sera za Trump kuhusu Palestina hususan uamuzi wake wa kuhamishia ubalozi wa Marekani huko Quds hapo tarehe 4 Mei, siku iliyosadifiana na wakati wa kukumbuka tukio la kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina inayojulikana kama Siku ya Maafa, ni ishara kwamba watu wa Mashariki ya Kati wataendelea kukabiliwa na taathira mbaya za sera za maafa ya Marekani na Israel.

Watoto wa Ukanda wa Gaza wanateswa kwa dhambi gani?

Baada tu ya Rais wa Marekani kutangazsa uamuzi wake wa kuitambua Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan yalikumbwa na machafuko makubwa na mapigano kati ya Wapalestina na askari wa utawala vamizi wa Israel. Wimbi jipya la malalamiko ya Wapalestina lililopewa jina la Intifadha ya Tatu limewatia wahka na wasiwasi mkubwa viongozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni.

Katika mazingira hayo Israel na kwa ruhusa ya Marekani ambayo ina uzoefu wa kukandamiza mataifa mbalimbali bali hata kuwakandamiza raia wake wenyewe hususan ukandamizaji wenye misingi ya kibaguzi, inaendelea kupanga na kutekeleza ramani na njama zake huko Palestina. Matokeo ya siasa na sera hizo ni mauaji zaidi ya raia wasio na hatia yanayofanywa na askari wa Israel huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.