Kususiwa sherehe za ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Quds
Zaidi ya nusu ya viongozi wa kigeni walioalikwa kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Quds, wamekataa kushiriki sherehe hizo.
Katika hali ambayo umesalia muda mfupi kabla ya kufanyika sherehe za ufunguzi wa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda mji wa Quds, kati ya wanadiplomasia 86 walioalikwa kushiriki sherehe za ufunguzi huo, ni wanadiplomasia 30 pekee waliotoa jibu chanya la kushiriki. Kwa mujibu wa gazeti la utawala haramu wa Israel la Haaretz, nchi ambazo zimetangaza wazi kwamba hazitoshiriki sherehe hizo ni pamoja na Australia, Ujerumani, Ireland, Malt, Mexico, Ureno, Poland, Russia, Sweden na Misri. Tarehe sita Disemba mwaka jana Rais Doanald Trump wa Marekanbi na licha ya kuwepo upinzani mkubwa wa kieneo na kimataifa, aliutangaza mji wa Quds, kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni.
Aidha Washington ilitangaza tarehe 14 ya mwezi huu kuwa siku ya kuuhamishia ubalozi wake kutoka Tel Aviv kwenda mji huo. Hatua hizo zimekabiliwa na maandamano makubwa ya Wapalestina na kadhalika radiamali kali kutoka nchi mbalimbali duniani juu ya njama mpya za Marekani na utawala haramu wa Kizayuni kuhusu mji huo. Kufuatia hatua hiyo ya Marekani kuutambua mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel, tarehe 21 Disemba mwaka jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa sambamba na kupitisha azimio, lilitangaza kwamba, halitoutambua mji huo kuwa mji mkuu wa Israel. Aidha Wapalestina sambamba na kulaani hatua hiyo ya kichochezi ya Marekani, walitoa mwito wa kususiwa sherehe za kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda mji huo.
Gazeti la Al-Quds Al-Arabi liliandika katika mtandao wake kwamba: "Viongozi wa Palestina wamewataka wawakilishi wa nchi tofauti, mabalozi na wanadiplomasia na asasi mbalimbali za kiraia kususia sherehe hizo za ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Quds." Hatua ya Trump ya kuutambua mji wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala pandikizi wa Kizayuni na maamuzi yake ya kuhamisha ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv kwenda mji huo, imeonyesha ni kwa kiasi gani Marekani ilivyo na chuki na uadui wa mkubwa dhidi ya Wapalestina na Waislamu. Aidha hatua ya Trump ya kupenda makubwa kupitia vitisho na ahadi, inakusudia kuwashinikiza Wapalestina na jamii ya kimataifa kujisalimisha mbele ya siasa zake za kimabavu. Kuwashinikiza Wapalestina kurejea tena kwenye meza ya mazungumzo eti ya maridhiano mkabala wa kuendelea kupatiwa misaada ya fedha na kadhalika kukatiwa misaada hiyo shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), ni sehemu ya siasa za uhasama zinazotekelezwa na Trump dhidi ya Wapalestina na ambazo zinaonyesha kiwango cha juu cha uadui alionao rais huyo dhidi ya taifa madhlumu la Palestina.
Lengo kuu la hatua hizo za kiuhasama za Marekani, ni kuwafanya Wapalestina waachane na suala muhimu la ardhi yao sambamba na kulifuta kabisa katika fikra za walimwengu, ili kufanikisha utekelezwaji wa siasa za utawala ghasibu wa Kizayuni kwa ajili ya kupanua wigo wa vitongoji na hatimaye kuuyahudisha kabisa mji wa Quds. Kwa kuzingatia matukio ya Palestina hasa baada ya kuingia madarakani Rais Trump, tunaweza kusema kuwa hatua za utumiaji mabavu na ukatili uliokithiri za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina, zimeshika kasi zaidi kutokana na mienendo mibaya ya Trump na uungaji mkono wake wa kila upande kwa utawala huo katili. Ukweli ni kwamba kila hatua ya Trump, imewazidishia masaibu na matatizo makubwa Wapalestina. Hata hivyo, jambo jema linalotokana na hali hiyo ni kuwabainikia wazi walimwengu malengo machafu ya Washington ambayo imekuwa ikiyaficha kwa muda mrefu.
Aidha kwa kuzingatia unyeti wa suala la Quds kwa Wapalestina, ulimwengu wa Kiislamu na fikra za waliowengi duniani kwa ujumla, harakati yoyote ya Marekani kuziunga mkono siasa za kupenda kujitanua za utawala katili wa Kizayuni katika mji wa Quds, bila shaka zitakabiliwa na radiamali hasi. Ni wazi kuwa kususiwa sherehe za ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Quds, kunabainisha kuendelea kutengwa nchi hiyo katika uga wa kimataifa hata na nchi washirika wake wa karibu.