Rais wa Uturuki: Israel inaisukuma Mashariki ya Kati kwenye lindi la vita
(last modified Mon, 14 May 2018 03:06:37 GMT )
May 14, 2018 03:06 UTC
  • Rais wa Uturuki: Israel inaisukuma Mashariki ya Kati kwenye lindi la vita

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unapanda mbegu za hofu na kulisukuma eneo la Mashariki ya Kati kwenye lindi la vita.

Erdoğan ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na kanali ya televisheni ya Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kwa mnasaba wa kukaribia safari yake ya kuitembelea Uingereza.

Rais wa Uturuki amekosoa mashambulio ya anga yaliyofanywa hivi karibuni na utawala haramu wa Israel katika maeneo kadhaa ya ardhi ya Syria na kusisitiza kuwa Israel imekuwa kila mara ikiwasha moto wa vita na hofu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Erdoğan amekadhibisha pia madai ya Israel kwamba miinuko inayoikalia kwa mabavu ya Golan ambayo iko kilomita 70 kutoka mji mkuu wa Syria, Damascus ilishambuliwa kwa makombora ya Iran na kubainisha kuwa, katika siku za karibuni, Syria imetangaza mara kadhaa kuwa makombora yaliyorushwa kuelekea Golan yalikuwa jibu la jeshi la nchi hiyo kwa mashambulio yaliyofanywa na Israel katika mji wa Qunait'ra.

Katika mahojiano hayo na BBC, Rais wa Uturuki vilevile ametahadharisha juu ya matokeo hasi ya kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kueleza kwamba uamuzi huo uliochukuliwa na rais wa nchi hiyo Donald Trump utasababisha matatizo katika siku za usoni.

Erdogan ameelekea nchini Uingereza kwa safari rasmi ya siku tatu ambako anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo juu ya masuala mbalimbali ya kieneo na kimataifa.../