Arab League yajitutumua, yataka kufanyika uchunguzi kuhusu jinai za Mazayuni
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ametaka kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na jinai za hivi karibuni za utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Ahmed Aboul Gheit ameyasema hayo Alkhamisi ya jana katika marasimu ya ufunguzi wa mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiarabu kilichofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri na kusema kuwa, ni lazima kufanyike uchunguzi wa kimataifa na wenye itibari kuhusiana na jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.
Aboul Gheit ameashiria kwamba, katika kipindi cha wiki moja pekee kwa akali Wapalestina 90 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya askari wa Kizayuni katika mpaka wa Gaza na kusema: "Tunataka ufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na jinai za askari wa Israel." Aidha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema: "Hii leo tunashuhudia ukiukaji wa wazi wa misingi ya sheria na maazimio ya Umoja wa Mataifa, kupitia kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Baitul-Muqaddas sambamba na kuongezeka mashambulizi na utumiaji nguvu mkubwa na jinai za askari wa Israel katika kukabiliana na maandamano ya amani ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza."
Amesema, kwa mara nyingine Jumuiya ya Nchi za Kiarabu inasisitiza kuwa maamuzi ya Marekani ya kuhamisha ubalozi wake Tel Avivi na kuupeleka mji wa Quds, ni maamuzi batili, ya kupingwa na kwamba uamuzi huo unakataliwa na jamii ya kimataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuanzia sasa na hata baadaye. Ahmed Aboul Gheit ameendelea kusema kuwa, maamuzi yasiyo ya uwajibikaji ya Marekani yameliingiza eneo la Mashariki ya Kati katika awamu mpya ya migogoro na mizozo zaidi. Kauli ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imetolewa katika hali ambayo baadhi ya nchi muhimu za jumuiya hiyo ni washirika wakubwa wa utawala wa Kizayuni suala ambalo ndilo limeufanya utawala huo katili kupata kiburi cha kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.