Mwaka mmoja wa mgogoro kati ya nchi za Kiarabu
(last modified Wed, 06 Jun 2018 05:57:20 GMT )
Jun 06, 2018 05:57 UTC
  • Mwaka mmoja wa mgogoro kati ya nchi za Kiarabu

Umetimia mwaka mmoja tokea uanze mgogoro baina ya nchi za Kiarabu na dalili zote zinaonyesha kuwa mgogoro huo ungali unaendelea bali hata utazidi kupanuka na kuwa mbaya zaidi.

Juni 5 mwaka 2017, nchi nne za Kiarabu yaani Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu  (UAE), Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar sambamba na kuiwekea vikwazo na mzingiro wa pande zote nchi hiyo. Miezi kadhaa baada ya kuanza mgogoro huo, zilionekana dalili za Qatar kuibuka mshindi katika msuguano ulokuwa umejitokeza.

Dalili ya kwanza ni kuwa, Qatar imefanikiwa kuvuka kizingiti cha taathira za kisaikolojia na za kifedha  za mzingiro huo na hata imeweza kukidhi mahitaji yake kinyume na ilivyotarajiwa.

Mfuko wa Kimataifa wa Fedha, IMF, mwezi Machi mwaka 2018 ulichapisha ripoti iliyosema kuwa, taathira za vikwazo dhidi ya Qatar ni ndogo na wala si kama ilivyodhaniwa na kwamba nchi hiyo 'imevuka' taathira hasi za vikwazo hivyo.

Dalili nyingine ya ushindi wa Qatar katika mgogoro huo ulioibuliwa na Saudia na waitifaki wake ni kuwa, nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi imeweza kuhuisha uhusiano na nchi kadhaa. Nchi kama vile Chad, Sudan na Jordan ambazo awali zilikuwa zimeifuata Saudia kibubusa katika kukata uhusiano na Qatar, katika kipindi cha chini ya miezi sita zilianzisha tena uhusiano wao na nchi hiyo. Kwa msingi huo njama ya Saudia ya kuzishawishi nchi zaidi za Kiarabu na Kiislamu ziisusie Qatar ziligonga mwamba. Hali kadhalika kuhuishwa uhusiano wa Qatar na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni dalili nyingine ya wazi ya kufeli mkakati wa Saudi katika mgogoro huo unaotokota baina ya nchi za Kiarabu.

Doha

Ikumbukwe kuwa mwaka 2015, Qatar ilijiunga na Saudi Arabia katika kukata uhusiano na Iran. Lakini Agosti mwaka 2017, Qatar ilimrejesha balozi wake mjini Tehran hatua ambayo ilihesabiwa kuwa ni kufeli sera za Saudia dhidi ya Iran katika eneo. Hivi sasa mgogoro huo wa Ghuba ya Uajemi  unaingia mwaka wake wa pili huku kukiwa na tetesi kuhusu njama za Saudia za kutekeleza oparesheni za kijeshi dhidi ya Qatar.

Gazeti la Kifaransa la Le Monde toleo la Juni Mosi liliandika: "Mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudia amemuandikia barua Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na kumfahamisha kuwa, iwapo Qatar itanunua mfumo wa ngao ya makombora ya S-400 kutoka Russia, basi Saudia itachukua hatua za kijeshi dhidi ya nchi hiyo jirani."

Matamshhayo ya mfalme wa Saudia yana nukta mbili za kuzingatiwa. Awali ni kuwa Saudi Arabia imeingiwa na hasira na ghadhabu kutokana na kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Qatar haijasalimu amri na inasisitiza kuhifadhi uhuru na mamlaka ya kujitawa. Msimamo huo wa Qatar unaweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi zingine za Kiarabu katika kusimama kidete mbele ya sera za mabavu za Saudia.

Tayari nchi kadhaa za Kiarabu kama vile Oman na Kuwait, ambazo ni wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, zimekataa kushirikiana na Saudia, Bahrain na Imarati dhidi ya Qatar. Huu ni mfano wa wazi kuwa nchi zingine za Ghuba ya Uajemi zinachukua sera huru zinazokinzana na matakwa ya Saudia. Nukta ya pili ni kuwa, mgogoro huo baina ya nchi hizo za Kiarabu unaingia katika mwaka wake wa pili huku kukiwa na wasi wasi kuwa yamkini hali ikawa mbaya zaidi baina ya nchi hizo katika siku za usoni.

Pamoja na hayo, nukta muhimu hapa ni kuwa, kinyume na madai ya Mfalme Salman kuwa nchi yake itachukua hatua dhidi ya Qatar, ukweli ni kuwa itakuwa vigumu kutekeleza kivitendo vitisho hivyo. Hii ni kwa sababu iwapo Saudia itaanzisha vita dhidi ya Qatar itakuwa haipigani tu na nchi hiyo bali itakuwa imeingia vitani na nchi kama vile Uturuki ambayo ina wanajeshi wake Doha kwa lengo la kuilinda nchi hiyo. Aidha itakuwa vigumu kwa Saudia kujiingiza vitani na Qatar kwani tayari jeshi lake limekwama katika kinamasi nchini Yemen na limeshindwa kufikia malengo yake.

Rais Erdogan wa Uturuki akiwa safarini nchini Qatar baada ya nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Saudia pamoja na waitifaki wake

Kuhusiana na hilo "Mujtahid", mwanaharakati katika mitandao ya kijamii ambaye mara kwa mara hufichua siri za Saudia amesema kuwa kumeshuhudiwa Saudia ikijaribu kujipenyeza Qatar kwa njia za angani, baharini na nchi kavu. "Mujtahid", katika ukurasa wake wa Twitter amesema hatua hizo za  Saudia zinashangaza kwani wakuu wa Riyadh wanafahamu udhaifu wao wa kijeshi na wanafahamu kuwa chokochoko yoyote itakuwa na matokeao mabaya kwao. Inavyoelekea ni kuwa katika kipindi hiki cha kuingia mwaka wa pili wa mgogoro baina yake na Qatar, Saudi Arabia inajaribu kuchochoea upinzani wa ndani ya nchi dhidi ya Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani na kuibua mgogoro katika familia inayotawala ili kuandaa mazingira ya mapinduzi dhidi ya kiongozi huyo.

Tags