HAMAS yatoa jibu la haraka na zito kwa mashambulizi ya Israel
Harakati ya Muqawama wa Palestina HAMAS, imetoa jibu kali na la haraka kufuatia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni yaliyotekelezwa na ndege za kivita za utawala huo eneo la Gaza asubuhi ya leo.
Katika jibu hilo, harakati ya HAMAS imevurumisha makombora yasiyopungua 20 kwenda vitongoji kadhaa vya utawala wa Kizayuni vya Sderot, Karam Abu Salem, Eshkol, pwani ya Ashkelon, Nahal Oz na maeneo mengine ya utawala huo katili. Utawala wa Kizayuni umekiri kwamba kwa akali makombora 20 na maguruneti kutoka ukanda wa Gaza yamevilenga vitongoji vyake kadhaa vya walowezi.
Hii ni katika hali ambayo muqawama wa Palestina umesisitiza kwamba kuanzia sasa hujuma yoyote ya Israel itajibiwa vikali na wanamapambano wa Palestina. Msemaji wa Harakati ya Palestina HAMAS, Fawzi Barhoum amesema kuwa, muqawama unaamini kwamba kutoa jibu kali na la haraka, kutaufanya utawala huo vamizi wa Kizayuni kusimamisha jinai zake. Ameongeza kwamba, kuwatetea raia wa Palestina, ni takwa la kitaifa na chaguo pekee la kistratijia kwa ajili ya muqawama. Asubuhi ya leo ndege za kivita za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia maeneo kadhaa ya muqawama eneo la Gaza.