Kupitishwa sheria ya kibaguzi zaidi katika bunge la Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46900-kupitishwa_sheria_ya_kibaguzi_zaidi_katika_bunge_la_israel
Kupitishwa sheria inayojulikana kama 'Nchi ya Taifa la Mayahudi' na 'Knasset" bungel la utawala haramu wa Israel, kumekabiliwa na upinzani pamoja na malalamiko makubwa ya taasisi, mashirika na jumuiya za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2018 08:04 UTC
  • Kupitishwa sheria ya kibaguzi zaidi katika bunge la Israel

Kupitishwa sheria inayojulikana kama 'Nchi ya Taifa la Mayahudi' na 'Knasset" bungel la utawala haramu wa Israel, kumekabiliwa na upinzani pamoja na malalamiko makubwa ya taasisi, mashirika na jumuiya za kimataifa.

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kupitishwa kwa sheria hiyo ya ubaguzi wa rangi na kusema kuwa inapingana moja kwa moja na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Licha ya kuwepo malalamiko mengi ya Mayahudi lakini bunge la utawala haramu lilipitisha mswada wa sheria hiyo siku ya Alkhamisi. Kwa mujibu wa sheria hiyo, ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo (Israel) zinachukuliwa kuwa ni za Mayahudi pekee na kwamba Wapalestina wanaoishi katika ardhi hizo watanyimwa haki zote za kiraia na za kibinadamu. Vilevile lugha ya Kiibrania ndiyo itakayokuwa lugha rasmi katika ardhi hizo. Sheria hiyo licha ya kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala huo ghasibu, inatambua ujenzi na kupanuliwa kwa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi kuwa thamani ya kitaifa na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuimarisha vitongoji vilivyopo sasa na kujengwa vingine vipya.

Knesset, bunge la utawala haramu wa Israel

Sheria hiyo ya kibaguzi imepitishwa katika hali ambayo kabla ya kupitishwa kwake maelfu ya wakazi wa Tel Aviv katika ardhi zinazokaliwa kwa mabvu walifanya maandamano makubwa ya kuupinga na vilevile Mayahudi wa Marekani wakaupinga vikali na kutaka usipitishwe na Knesset kwa hoja kuwa ni wa ubaguzi wa rangi. Licha ya upinzani huo mkali lakini viongozi wa Wazayuni wameupitisha kwa lengo la kufikia malengo yao ya kibaguzi na kichokozi katika ardhi za Wapalestina wanazozikalia kwa mabavu. Kupitia sheria hiyo, watawala wa Kizayuni wana lengo la kudumisha mpango wa kutekeleza mauaji ya kizazi, kuwalazimisha wapalestina kuhama ardhi zao, kueneza mradi wa kubadilisha muundo wa kijamii wa Palestina na kuufanya uwe ni wa Kiyahudi, kudumisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kusimamisha mpango wowote wa kuwawezesha wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika radhi zao za jadi. Kwa hakika sheria hiyo ni kudumishwa turathi ya kikoloni na ya ubaguzi wa rangi ambayo imejengeka katika msingi wa mauaji ya kizazi, kufutwa taifa la Palestina na kupuuzwa haki zao zote za msingi. Kuhusiana na suala hilo Swaib Arikaat, Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina PLO amesema kuwa sheria hiyo ni udumishwaji wa turathi ya kikoloni ambayo imesimama kwenye msingi wa mauaji ya kizazi na kupuuza kwa makusudi, haki za wakazi asilia wa ardhi hizo za kihistoria.

Umoja wa Ulaya umelaani sheria mpya ya kibaguzi ya Israel

Hata kama hatua hizo za kinyama na za kibaguzi za utawala wa Kizayuni zimekuwa zikitekelezwa kwa miaka mingi dhidi ya Wapalestina, lakini zimepata kasi na msukumo mpya kutokana na uungaji mkono mkubwa inauopata utawala huo kutoka kwa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani. Hivi majuzi Trump aliuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Quds (Jerusalem) kutoka Tel Aviv na vilvile kuiondoa nchi yake Katika Baraza la Haki za Binadamu katika kuinga mkono Israel na hivyo kuthibitisha kivitendo kuwa nchi hiyo ni mshirika na muungaji mkono mkuu wa utawala huo wa kibaguzi unaoendelea kutenda jinai za kutisha dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina. Fauzi Barhum, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina anasisitiza kuhusu suala hilo kwamba kama kisingekuwa ni kimya cha nchi za eneo na uungaji mkono mkubwa wa Marekani kwa jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina, kamwe sheria hiyo ya kibaguzi haingepitishwa.

Trump, muungaji mkono mkubwa wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Kupitishwa kwa sheria hiyo inayotajwa kuwa 'Taifa la Mayahudi', bila shaka ni mfano mwingine wa wazi wa ubaguzi wa rangi na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina na vilevile kukanyagwa misingi ya sheria za kimataifa. Ahmad Tibi mbunge katika Knesset ya Israel anasema kuwa kupasishwa kwa sheria hiyo ni kuuawa demokrasia katika ardhi za Palestina.