Jul 30, 2018 11:07 UTC
  • Kusambaratika uchumi wa Bahrain katika kivuli cha utawala wa Aal Khalifa

Ripoti mbalimbali kutoka nchini Bahrain zinaonyesha kuwa, hali ya uchumi wa nchi hiyo ya Kiarabu inazidi kuwa mbaya chini ya kivuli cha utawala wa Aal Khalifa.

Kuzorota siku baada ya siku uchumi wa Bahrain kumeakisiwa pakubwa na vyombo mbalimbali vya habari huku wataalamu wa masuala ya kiuchumi na waandishi amilifu wa habari katika uga wa uchumi nchini humo wakiaendelea kutoa tahadhari kuhusiana na mwenendo mbaya wa uchumi wa nchi hiyo. Adel al-Marzouq mwandishi wa habari wa Bahrain anatabiri kwamba: Miaka michache ijayo uchumi wa nchi hiyo utasambaratika na kuporomoka kabisa. al-Marzouq ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Mzigo mkubwa wa madeni ya Bahrain, nakisi ya bajeti na riba ya madeni hayo ni sawa na nusu ya bajeti ya nchi hiyo.

Ripoti zinaonyesha kuwa, deni la Bahrain kwa sasa limefikia dola bilioni 40 na inatabiriwa kwamba, litaongezeka na kufika dola bilioni 50. Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, filihali Bahrain inakabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2009.

Hamad bin Issa Aal Khalifa, mfalme wa Bahrain

Inatabiriwa kuwa, mwenendo wa kuongezeka madeni kwa nchi za Kiarabu utaendelea hadi mwaka 2020 na kwamba, Bahrain itageuka na kuwa nchi yenye madeni mengi zaidi miongoni mwa nchi za Kiarabu.

Watawala wa Bahrain kutokana na kuhofia malalamiko na hisia za fikra za waliowengi katika nchi yao walikuwa wakizuia kufichuliwa habari za hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo ambayo ni matokeo ya uongozi mbaya wa watawala wa nchi hiyo pamoja na siasa za kijeshi, ukandamizaji, kupenda vita na kuingilia mambo ya nchi nyingine.Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana kuanzia Juni mwaka 2015 hadi sasa viongozi wa Manama wamekataa kutoa takwimu za aina yoyote zinazohusiana na uchumi wa nchi hiyo. Ukweli wa mambo ni kuwa, natija ya miaka mingi ya utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa nchini Bahrain si kitu kingine bighairi ya kudorora uchumi na kuifanya nchi hiyo kuwa tegemezi kwa nishati ya mafuta.

Gazeti la al-Quds al-Arabi linalochapishwa mjini London Uingereza limeandika katika moja ya makala zake kwamba, kati ya nchi za Kiarabu wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, Bahrain daima imekuwa na ingali inakabiliwa na vurugu za kisiasa na kulegalega uchumi wake.

Hali ya uchumi hivi sasa ya nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi ikiwemo Bahrain chimbuko lake hasa ni nchi hizo kufuata kibubusa siasa zisizopima mambo za Saudi Arabia kuhusiana na masuala mbalimbali.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa Aal Khalifa

Hatua ya Saudi Arabia ya kutumia nishati ya mafuta kama silaha dhidi ya wapinzani wake na madola yasiyokubali kuburuzwa kama Russia, Iraq na Iran ni miongoni mwa mambo ambayo madhara yake yamezirejea zaidi nchi hizo zenyewe na nchi nyingine za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ambazo uchumi wao unategea nishati ya mafuta.

Fedha nyingi zinazotumiwa na wana mfalme wa nchi za Kiarabu katika anasa na starehe, kuwalipa mishahara magaidi wa kukodi huko Syria na Iraq, gharama kubwa ya utawala wa Aal Saud katika vita huko nchini Yemen, siasa zao mbovu za kiuchumi na bajeti kubwa za kununua silaha mbalimbali zinazotengwa na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ni mambo ambayo yamechangia pakubwa katika kuzorota na kusambaratika uchumi wa nchi hizo. Hii ni katika hali ambayo, kwa mwaka Bahrain hutenga fedha nyingi mno kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la siasa zake za ukandamizaji dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Kuendelea siasa za utawala wa Aal Khalifa zilizo dhidi ya wananchi katika uga wa kisiasa, kijamii, kiuchumi na kadhalika kumekuwa na matokeo hasi na mabaya na kuzidi kuharibu maisha ya wananchi hao hasa katika suala zima la uchumi. Kwa muktadha huo, uongozi wa Aal Khalifa kivitendo umeufanya uchumi wa Bahrain kufikia katika kiwango cha mgogoro na kuweko kila ishara za kufilisika na kusambaratika uchumi wa nchi hiyo.

Tags